Asubuhi ya leo, katika jiji lenye pilikapilika la Dar es Salaam, viongozi, wataalamu, na wakandarasi walikusanyika kwenye ukumbi mkubwa wa Mlimani City kusherehekea maadhimisho ya 21 ya Siku ya Wakandarasi.
Siku hii adhimu Ilichangamka kama ilivyotarajiwa, lakini ilibeba uzito wa hoja kali na kuibua changamoto zinazoikumba sekta ya ujenzi nchini.
Waziri wa Ujenzi, Mh. Innocent Bashungwa, akiwa katika jukwaa mbele ya halaiki ya wataalamu wa ujenzi, alitoa hotuba iliyojaa ukakamavu.
Akiwa na sura ya umakini, alikemea kwa nguvu tabia ya baadhi ya wakandarasi ambao, mara baada ya kusaini mikataba na kupokea malipo ya awali, hukwepa majukumu yao. “Kuna wimbi la wakandarasi ambao baada ya kupata (Advance Payment) , wanaanza kusumbua na kushindwa kutimiza ahadi zao,” alieleza Waziri Bashungwa kwa sauti yenye msisitizo.
Maneno yake yalikuwa kama kengele ya tahadhari kwa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB), akikazia kuwa ni lazima isimamie kwa makini tabia na utendaji wa wakandarasi ili kuepusha ubabaishaji unaoleta hasara kubwa kwa taifa.
Katika hotuba yenye kuwaasa wakandarasi hao, hakuwa peke yake. Katibu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhandisi Zena Said, naye alichukua nafasi yake kutoa wito kwa wahandisi kutendea haki viapo vyao vya taaluma.
“Wahandisi lazima wawe waadilifu, wafuate uzalendo na kufanya kazi kwa umakini ili kuleta maendeleo ya kweli,” amesema kwa sauti yenye hekima, ikionyesha dhamira yake ya kuona wahandisi wanakuwa sehemu ya suluhisho na si tatizo.
Msajili wa Bodi ya Usajili Wahandisi Tanzania (ERB), Mhandisi Bernard Kavishe, alichukua nafasi hiyo kuelezea mipango ya bodi katika kuimarisha sekta hiyo. “Tumeendelea na mpango wetu wa STEM ili kuwaandaa wahandisi wetu kwa fursa mpya zinazokuja,” amesema Mhandisi Kavishe, akimaanisha mpango wa kuhamasisha masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi, na hisabati ili kuongeza nguvu kazi yenye weledi na ubunifu wa sayansi ya kisasa.
Maadhimisho hayo yamebeba kauli mbiu ya kuvutia, “Kuweka Nguvu Kazi ya Uhandisi kwa Enzi Akili Mnemba,” ikimaanisha umuhimu wa kutumia akili, maarifa, na teknolojia ili kufanikisha miradi yenye ufanisi na ubora.