Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Zainab Katimba amesema Serikali itaendelea kutenga fedha ya ukarabati wa barabara korofi nchini zilizoathiriwa na Mvua za El – Nino ili kurahisisha huduma bora kwa Wananchi.
Mhe. Katimba amesema hayo katika kipindi cha maswali na majibu Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo Hai Mhe. Saashisha Mafue, aliyeuliza Je, lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mhe. Rais ya kujenga barabara ya Sadala hadi Uswaa kwa kiwango cha lami?
Amesema katika mwaka 2023/2024 barabara hiyo ilifanyiwa matengenezo ya sehemu korofi kwa gharama ya shilingi Milioni 26.8 na mwaka 2024/2025 shilingi Milioni 35 zimetengwa kwa ajili ya kufanya ukarabati katika maeneo yote korofi kote nchini.
Amesema Serikali kupitia wakala wa barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika mwaka wa fedha 2024/2025 imepanga kufanya usanifu wa kina kwa Kilomita zote 9.87 za barabara ya Sadala Uswaa kwa lengo la kutambua gharama halisi zitakazotumika katika kuijenga barabara hiyo mara baada ya usanifu kukamilika na gharama halisi za ujenzi kujulikana Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami.