NA FAUZIA MUSSA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kuwa washirika wa kimkakati katika kuboresha mazingira ya kazi, fursa sawa za maendeleo kwa wanawake wahasibu ili kuandaa viongozi bora wanaotokana na wanawake wa hasibu hapo baadae.
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah wakati akimwakilisha kuzindua kongamano la saba la Uongozi la Wanawake Wahasibu Tanzania , alisema Serikali inatambua umuhimu wa kuwekeza katika elimu, mafunzo na kuondoa vikwazo dhidi ya wanawake ili kufikia ndoto zao za kiuongozi.
Dk.Samia alisema kongamano hilo ni chachu ya kukumbushana kuhusu thamani ya uwezo wa asili wa mwanamke, hivyo kuwataka kutumia nguvu zilizomo ndani yao kikamilifu, ili kufikia malengo ya chama hicho
Alisema uzowefu unoanesha kuwa maendeleo ya kweli na endelevu yanapatikana endapo sauti na mchango wa wanawake vinapewa uzito unaostahili kijamii, kiuchumi na kisiasa, hivyo aliwataka wanawake hao kulitumia kongamano hilo kwa kujenga mtandao imara wa kusaidiana na kuhamasishana kuelekea malengo ya pamoja.
Akitoa taarifa ya chama cha wanawake wahasibu TanzaniaTAWCA, Mwenyekiti wa baraza la uongozi TAWCA, CPA Dk. Neema Kiure alisema chama hicho mbali ya kuhamasisha wanawake kujiunga katika fani ya uhasibu lakini pia kimekua na kazi mtambuka ya kuhudumia jamii kuhusu masuala ya jinsia , kutoa ushauri wa kitaalamu wa stadi za maisha na ujasiriamali ambapo wamewafikia wajasiriamali wadogowadogo hasa makundi maalum kuwafundisha matumizi bora ya mikopo wanayopewa na Serikali ili kupunguza kiwango cha mikopo isiyolipika, kupitia mradi wa bado na weza
“TAWCA imefanikiwa kuwapatia mafunzo wasichana 101 waliopata mimba za utotoni, na wengi wao wamefanikiwa kujiwezesha kiuchumi kwa kuanzisha na kuendeleza biashara zao binafsi.” Alisema
Aidha alisema chama hicho kina mpango wa kushirikiana na serikali katika kupunguza umaskini ambapo kimefanikiwa kuwaunganisha wahasibu Zaidi ya 1000 kushiriki katika harakati za kumkoomboa mwanamke kielimu na kiuchumi nchini.
Alifahamisha kuwa kufanyika kwa makongamano kama hayo kunasaidia kuimarisha maendeleo ya uongozi,kukuza usawa wakijinsia,na kuwawezesha wanawake kujiamini kushindana na vikwazo vya maendeleo ya wanawake.
Mkurugenzi mtendaji wa chama hicho,CPA Tumain Laurance alisema kongamano hilo ni la saba kufanyika tangu kuasisiwa mwaka 2018 namafanikio mbalimbali yamepatikana kupitia makongamano hayo.
Alisema miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuongeza idadi ya wahasibu wanawake nchini ambapo mwaka 2015 wahasibu wanawake walikua asilimia 23 na kufikia asilimia 37 mwaka 2024, hali inayooneshwa mwamko wa wasichana kusoma masomo yahesabu na biashara.
Alisema ongezeko la wahasibu wanawake limechangiwa na kuondoa dhana ya wanafunzi kutopenda kusoma hesabu ambapo chama hicho kinaendelea na mpango wa kuhamasisha wasichana kusoma hesabu na masomo ya biashara ili kuongeza namba ya wahasibu wanawake nchini.
Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Mhe Juma Makungu Juma amesema Serikali inatambua mchango wa wanawake wahasibu nchini katika kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uaminifu mkubwa hivyo itaendelea kufanya kazi kwa karibu na TAWCA ili kufika malengo ya kuanzishwa kwa Chama hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa wahasibu na Wakaguzi wa hesabu Tanzania(NBAA) CPA Pius Maneno alisema chama hicho kilianzishwa mwaka 2015, chini ya kifungu cha sheria ya jamii ya mwaka 2002 ikiwa ni juhudi ya bodi ya taifa ya wahasibu na wakaguzi wa hesabu kwa lengo la kuhamasisha wanawake kujiunga kwenye fani ya uhasibu.
Aidha alieleza kuwa chama hicho kilianzia na wahasibu 18 na sasa kina jumla ya wanachama 1011, hali inayoonesha kukuwa kwa chama hicho siku hadi siku.
Kongamano hilo lililobeba kauli mbiu ‘nguvu iliyo ndani yako (the power of you)’ liliwashirikisha takribani wanawake 400 wa fani mbalimbali wakiwemo wahasibu, wakaguzi wa hesabu, rasilimali watu pamoja na utawala.