Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Novemba 12, 2026
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Pwani, Richard Kayombo, amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii katika halmashauri kusimamia kwa karibu vikundi vinavyonufaika na mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri ili kuhakikisha vinaitumia vizuri na kurejesha kwa wakati.
Aidha, amewataka wanufaika wa mikopo hiyo kuwekeza katika miradi yenye tija itakayowawezesha kukuza mitaji, kurejesha mikopo na kujiinua kiuchumi.
Akifungua kikao cha tathmini ya utoaji wa mikopo hiyo kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, kilichofanyika Kibaha, Kayombo amesema mafanikio ya mikopo hiyo yanapaswa kupimwa kwa kuangalia mabadiliko halisi ya maisha ya wanufaika.
Alisisitiza kuwa Maafisa Maendeleo ya Jamii hawapaswi kuishia kutoa mikopo pekee, bali wanapaswa kufuatilia vikundi, kutoa elimu ya uendeshaji wa biashara na kuhakikisha marejesho yanafanyika kwa wakati ili fedha hizo ziendelee kunufaisha vikundi vingine.
“Niwaombe Maafisa Maendeleo ya Jamii halmashauri kuwafuatilia wanufaika, siyo kuishia kuwapatia mikopo pekee, bali mhakikishe mnawapatia elimu ya uendeshaji wa biashara na urejeshaji uwe kwa wakati ili fedha hizo zinufaishe na wengine,” alisisitiza Kayombo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mikopo ya Asilimia 10 Mkoa wa Pwani, Mbonea Makenya, alisema katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027 jumla ya Sh bilioni 4.5 zimetolewa kwa vikundi 280 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, vikivyonufaisha watu 1,320.
Alisema hadi sasa jumla ya Sh bilioni 22 zinadaiwa kutoka katika mikopo iliyotolewa vipindi vya nyuma, huku Sh bilioni 2.4 zikiwa zimerejeshwa. Kati ya madeni hayo, Sh bilioni 15 zinadaiwa kwa vikundi vilivyo ndani ya mkataba na Sh bilioni saba kwa vikundi vilivyo nje ya mkataba.
Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Kibiti, Alex Dismas, alisema kikao hicho kimewapa fursa ya kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa mikopo hiyo, huku akiishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa mikopo kwa makundi hayo.
Alisema wilaya hiyo inadai Sh milioni 44 za mikopo iliyotolewa tangu mwaka 2024 na inaendelea na ufuatiliaji pamoja na kutoa elimu kwa wanufaika ili kuongeza ufanisi wa mikopo hiyo.

