Na Ashrack Miraji (Fullshagwe Media) Same Kilimanjaro
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro imetoa vyeti vya pongezi kwa Taasisi ambazo zimefanya vizuri kwenye ukusanyaji wa Mapato Wilayani humo, Taasisi hizo ni Mamla ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.
Moja ya Taasisi iliyofanya vizuri zaidi ni TRA ambao Katika kipindi cha robo mwaka ya nne yaani kuanzia mwezi April – June 2024 imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi Milioni mia nane sabini na moja, elfu sitini na moja, mia sita sabini na nane (871, 061, 678.00) makusanyo hayo ni ongezeko la shilingi Milioni mia moja tisini na tatu, laki tano tisini na saba, mia nne tisini na tisa na senti sabini na saba 193, 597, 499. 77 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 29% ikilinganishwa na makusanyo ya shilingi milioni mia sita sabini na saba, laki nne sitini na nne, mia moja sabini na nane na senti ishirini na tatu (677, 464, 178. 23) yaliyokusanywa katika kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha uliopita2022/23.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vyeti hivyo Mkuu wa Wilaya hiyo Kasilda Mgeni amepongeza jitihada mbalimbali zinazo fanywa na Taasisi hizo kwenye ukusanyaji wa Mapato, huku akisisitiza kuendelea kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa bidii ili waweze kufanya vizuri zaidi.
Aidha ili kuhakikisha Taasisi hizo zinatekeleza majukumu yao kwa ufanisi kumeanzishwa kikao maalumu cha kujadili mwenendo wa ukusanyaji wa mapato cha Wilaya ya Same ambacho kinalenga kushauriana namna ya kuweza kufikia lengo la ukusanyaji wa mapato, lakini pamoja na kutatua changamoto na malalamiko yanayojitokeza wakati maafisa wanapotekeleza majukumu yao ya msingi kisheria ya ukusanyaji wa mapato.
Kikao hicho maalum kinajumuisha wajumbe kutoka kwenye taasisi zinazokusanya mapato kwenye Wilaya ikiwemo Mamla ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Wakala wa usamabazaji maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) na Halmashauri.