Na. Dennis Gondwe, DODOMA
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma limepokea taarifa ya ufungaji wa hesabu kuishia tarehe 30 Juni, 2024 na
kushauri kuwa changamoto zilizojitokeza katika mwaka ulioishika zitatuliwe ili zisijitokeze katika ufungaji hesabu ujao.
Baada ya taarifa ya ufungaji wa hesabu kuishia tarehe 30/6/2024 kuwasilishwa kwenye mkutano maalum wa Baraza
la Madiwani kwa ajili ya kupitia na kujadili taarifa ya ufungaji wa hesabu iliyowasilishwa na Mkuu wa Kitengo cha Uhasibu na
Fedha Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wajumbe waliipokea.
Mwenyekiti wa Mkutano huo, Prof. Davis Mwamfupe aliwahoji wajumbe kama wanaipokea taarifa hiyo na kwa kauli moja
waliipokea taarifa hiyo. Alisema kuwa taarifa hiyo imehusisha mapendekezo ya Kamati ya Fedha na Utawala kama walivyoshauri.
Akiwasilisha taarifa ya ufungaji hesabu za halmashauri kuishia tarehe 30 Juni, 2024, Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu,
CPA David Rubibira alisema kuwa taarifa hiyo inatokana taarifa za fedha ambazo huwasilishwa kwenye vikao vya kamati ya
fedha na utawala kila mwezi.
Akiongelea umuhimu wa kuwasilisha taarifa hizo, alisema kuwa ni takwa la kisheria kuandaa hesabu kwa mfumo wa kimataifa yaani ‘International Public Sector Accounting Standard’ (IPSAS).
“Umuhimu ni takwa la kisheria kwamba unapomaliza mwaka wa fedha halmashauri inatakiwa kuwa na hesabu za
mwaka husika zilizowasilishwa kwa Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ndani ya kipindi cha miezi 3.
Kwa mujibu wa Kanuni ya Fedha ya Serikali za Mitaa ya mwaka 2009, kifungu cha 31 na kifungu namba 45 cha Sheria ya Serikali za
Mitaa ya mwaka 1982 na marejeo yake ya mwaka 2000 kinatutaka kuandaa hizo hesabu na kuziwasilisha. Hivyo,
baraza lako lazima lizipitie na kutoa maoni kwenye hizo hesabu ili tuziwasilishe kwa wakati” alisema CPA Rubibira.
Akiongelea maudhui ya taarifa hiyo, alisema kuwa inahusisha taarifa ya mali na madeni, mizania ya fedha, mapato na
matumizi na mtiririko wa fedha. Maeneo mengine aliyataja kuwa ni utendaji kazi wa menejimenti kwa kushirikiana na
madiwani, uhai wa halmashauri, taarifa hiyo inaonesha pia akaunti za halmashauri hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2024,
pamoja na mambo mengine.
Akichangia taarifa hiyo, Diwani wa Kata ya Chang’ombe, Bakari Fundikira alisema kuwa taarifa hiyo ni dira kwa mwaka wa fedha unaoendelea.
“Tumeipokea taarifa na kuipongeza timu ya wataalam kwa uandaaji mzuri wa taarifa. Taarifa imetupa dira ya mwaka huu wa fedha ambao tunao.
Yale mapungufu tukayafanyie kazi ili taarifa ya mwaka huu iwe bora zaidi na madeni yaweze kupungua kwa kiasi kikubwa. Taarifa hii itupe dira ya utekelezaji wa shughuli za halmashauri” alisema Fundikira.