Na Neema Mtuka, Rukwa.
Wadau wa sekta za umma binafsi na wananchi wametakiwa kuchangamkia fursa za maendeleo kwa kufanya uwekezaji mdogo, uwekezaji wa kati na mkubwa ndani ya Wilaya ya Sumbawanga ili kuleta maendeleo endelevu.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Baraza la biashara ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile
katika kikao cha baraza hilo la biashara wilaya ya Sumbawanga.
Ambapo katika kikao hicho wadau kutoka Taasisi za umma na binafsi wamejadili kwa kina hali ya maendeleo ya biashara na fursa za uwekezaji na kuona uhitaji mkubwa wa kuendelea kuchangamkia fursa za uwekezaji katika nyanja tofauti kama kilimo na ardhi.
Wakati akiongoza kikao Cha baraza hilo Chirukile amesema malengo ya Serikali ni kuhakikisha shughuli za biashara zinastawi ikiwa ni pamoja na kuendeleza fursa za uwekezaji katika nyanja zote za viwanda na shughuli za kibiashara katika kuufikia uchumi wa juu.
Ameongeza kuwa elimu juu ya fursa za uwekezaji inatakiwa kuwafikia wadau wa ndani na nje ili waweze kufanya uwekezaji wenye tija katika kuongeza uchumi wa Serikali na mtu mmoja mmoja.
Pia amewataka wananchi kuwekeza bila uoga na kuacha tabia ya kuona uwekezaji ni kwa ajili ya watu kutoka nje ya nchi.
“Wananchi acheni uoga changamkieni fursa mbalimbali zinazojitokeza na kujenga uchumi wa nchi”.Amesema Nyakia
Kwa upande wake katibu wa jumuiya ya wafanyabiashara mkoa wa Rukwa Henry Daudi Mwakalile amesema kuwa baraza hilo ni nyenzo muhimu na pekee maana inawaunganisha wadau kutoka Taasisi tofauti na kupeana ujuzi juu ya fursa zilizopo .
Amesema kuwa baada ya kuziona fursa ndipo unachukua hatua kufikia hatima ya uchumi mzuri kupitia uwekezaji wenye tija katika viwanda na biashara.
Nao baadhi ya wadau walioshiriki katika Baraza hilo wameitaka Serikali kuwakutanisha mara kwa mara na kuendelea kuwajengea uwezo ili kuyafikia maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan.
Hata Hivyo Mwakalile ameishukuru Serikali kwa kuandaa baraza hilo kwa kuwa litaendelea kuchochea shughuli za uwekezaji utakaopandisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.