Mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga
Bi Pendo Mangali
Na Neema Mtuka, Rukwa.
Wakuu wa shule za sekondari na maafisa elimu kata zilizopo ndani ya halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga wametakiwa kuongeza uwajibikaji katika kuinua taaluma na ufaulu kwa wanafunzi katika shule hizo.
Hayo yamesemwa katika kikao kazi cha mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga Bi Pendo Mangali na maafisa elimu sekondari na msingi viongozi wa tume ya utumishi wa walimu mipango fedha wakuu wa divisheni za utumishi mkaguzi wa ndani pamoja na wakuu wa shule za sekondari.
Mangali amewataka wahakikishe daraja sifuri zinakoma katika matokeo ya mitihani ya wanafunzi kwa kuongeza weredi katika uwajibikaji na kuandaa mikakati kwa kila shule itakayoongeza kiwango cha ufaulu.
Amesema kuwa kila mwalimu anatakikiwa kutimiza majukumu yake katika suala zima la ufundishaji na kujituma jambo ambalo litawafanya wanafunzi wapende kusoma.
Aidha pendo amewaasa walimu kuwa waaminifu wenye maadili na heshima kwa viongozi na utii kwa serikali ili kuwa mfano bora kwa wanafunzi na kwa jamii inayowazunguka.
“Mwalimu ni kiio cha jamii unapokuwa na heshima na maadili hata ukiwa unafundisha wanafunzi wanakupenda na hata kulipenda somo unalofundisha hivyo ni muhimu uadilifu wenu uwe mfano kwa jamii.”Amesema Mkurugenzi
Hata hivyo Mangali amewataka walimu hao kuwa na ushirikiano katika usimamizi wa miradi ya maendeleo katika kada ya elimu ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati.
Amesema kuwa miradi hiyo iwe na ubora kwa kuzingatia thamani ya fedha kama lilivyo lengo la serikali la ujenzi wa miundombinu ya elimu inayokidhi vigezo na viwango.
Sambamba na hayo wataalamu hao wamewasilisha changamoto zinazowakabili katika utendaji wa kazi zao na kupatiwa utatuzi wa papo hapo na Mkurugenzi.
Afisa elimu sekondari Manispaa ya Sumbawanga Hebel Kibona ameeleza kuwa walimu watajitoa kikamilifu kuandaa mashindano ya mitihani ya mara kwa mara ili kuongeza taaluma ya wanafunzi kama lilivyo lengo la serikali.