Na Masanja Mabula- Pemba
Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameutaaka uongozi wa Wizara ya utalii na Mambo ya kale kuhakikisha wanaongeza wigo katika kuboresha vivutio vya utalii vilivyopo Kisiwani Pemba kwa lengo la kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo katika Tamasha la Mswahili wa Kipemba lililofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Wete Pemba.
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane(8) inayoongozwa na Rais Dkt Hussen Mwinyi imeweka adhma kubwa ya kuifungua Pemba Kiuchumi kwa kupitia Sekta mbali mbali ikiwemo Sekta ya Utalii kwa wageni na wananchi wa kisiwa hicho .
Makamu wa pili wa Rais Zanzibar amesema kuwa Serikali imelipa kipaombele Suala la Utalii kwa maslahi mapana ya kukuza uchumi wan chi hivyo ni lazima kuhakikisha kuwa wanaimarisha Milla, silka na Utamaduni wa Mzanzibari kwa Maslahi mapana ya Nchi na vizazi vinavyokuja.
Aidha Mhe. Hemed amesema katika kufika Malengo iliyojiwekea ya kuifungua Pemba kiuchumi Serikali Inaendelea kuchukua hatua mbali mbali ikiwemo kuimarisha miundombinu ya barabara kwa kujenga Barabara kuu na Barabara za ndani ambapo zitakapokamili zitarahisisha usafiri wa wananchi na wageni pamoja na usafirishaji wa bidhaa na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Pia Makamu wa Pili wa Rais amesema Serikali inakamilisha taratibu za ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Pemba wenye hadhi ya Kimataifa kupitia kampuni ya PROPAV kutoka nchini Brazil ambao kukamilika kwake kutasaidia kukua kwa utalii kutokana na watalii kuingia moja kwa moja kutoka katika nchi zao na kufika katika kiswa cha Pemba.
Sambamba na hayo ameiagiza Wizara ya Utalii na mambo ya kale kuhakikisha wageni wanaoingia Unguja wanapata fursa ya kufika Kisiwani Pemba, kuongeza jitihada katika kuvitangaza vivutio vya utalii kwa Unguja na Pemba kwa ngazi ya Kitaifa na Kimataifa pamoja na kuwasimamia wamiliki wa Hoteli za Kitalii kununua bidhaa zinazozalishwa Unguja na Pemba ili kunyanyua soko la ndani la wajasiriamali.
Nae waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mhe.Mudrik Ramadhan Soraga amesema dhamira ya Tamasha la Mswahili wa Kipemba ni kuifungua Pemba kupitia Sekta ya Uwekezaji na Utalii ili wananchi waweze kutambua fursa zinazopatikana katika sekta ya Utalii.
Soraga amesema Pemba ni eneo la kimkakati katika Sekta ya Utalii hivyo kila mmoja kwa nafasi yake awe balozi wa kutangaza fursa za kiutalii zilizopo Pemba ili ziweze kutambulikana Kitaifa na Kimataifa sambamba na kudhamiria kuliendeleza na kuliboresha Tamasha la Mswahili wa Kipemba liweze kufanyika kila mwaka katika ubora wa hali ya juu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Zanzibar Ndugu RAHIM BALOO amesema Azma ya Serikali ni kuona Utali unakuwa na kuimarika zaidi kwa kudumisha Mila, Silka na Tamaduni za kipemba katika kuelekea kuifungua Pemba Kiutalii.
Amesema kuimarishwa kwa miundombinu mbali mbali nchini kumepelekea kuongezeka kwa idadi ya wageni wanaoingia Zanzibar kutoka Mataifa mbali mbali duniani jambo ambalo linaongeza thamani na hadhi ya Zanzibar.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais amepokea maandamano ya washiriki wa tamasha sambamba na kukagua Maonesho ya Tamasha la Mswahili ya kipemba yaliyofanyika katika viwanja vya Baraza la wawakilishi la zamani Wete.