*Yaongeza nguvu kinyang’anyiro nafasi ya Ukurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika
Na WAF – Congo, Brazaville
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahamoud Thabit Kombo, wamewasili Jijini Brazzaville nchini Congo wakiwa pamoja na ujumbe maalum wa Tanzania kwa ajili ya kumnadi mgombea wa Tanzania Dkt. Faustine Ndugulile (MB) katika nafasi ya Ukurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.
Timu hiyo imewasili leo Agasti 24, 2024 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 74 wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Katika mkutano huo muhimu, ujumbe wa Tanzania unajumuisha wataalamu na viongozi kutoka Wizara ya Afya, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wajumbe hawa wanatarajia kushiriki mikutano ya pembezoni ili kujadili masuala muhimu na kuhakikisha upatikanaji wa kura kutoka kwa nchi wanachama wapatao 47 wa WHO.
Ujumbe huu wa Tanzania unaratibiwa chini ya uenyekiti wa Mhe. Balozi Robert Kahendaguza kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa OR-TAMISEMI Dkt. Grace Magembe.
Miongoni mwa wajumbe wanaoshiriki kutoka Wizara ya Afya ni pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Dkt. Ntuli Kapolongwe.
Kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ujumbe unajumuisha pia mabalozi wenye uzoefu mkubwa, akiwemo Mhe. Balozi Noel Kaganda, Mhe. Balozi Mindi Kasiga, Mhe. Balozi Suleiman Haji, na Mhe. Balozi Hoyce Temu.
Aidha, ujumbe huo unapata nguvu kutoka kwa wajumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Mhe. Elibariki Emmanuel Kingu, Mhe. Neema Kichiki Lugangira, Mhe. Joseph Kizito Mhagama, Mhe. Shamsia Azizi Mtamba, na Mhe. George Ranwell Mwenisongole.
Juhudi hizi za Tanzania ni kielelezo cha dhamira thabiti ya nchi katika kuimarisha nafasi yake kwenye jukwaa la kimataifa hususan katika masuala ya Afya ambapo Mgombea Dkt. Ndugulile anatarajiwa kupigiwa kampeni kwa nguvu zote kutoka kwa timu ya Tanzania ili kuweza kushinda nafasi hii muhimu ambayo itailetea nchi yetu heshima kubwa.