Na Mwandishi wetu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi amewatahadharisha wananchi wa tarafa ya Ngorongoro kutokubali kutumika na mtu au vikundi vya watu wenye nia mbaya hususan kupitia baadhi ya mitandao ya kijamii kwani kwa kufanya hivyo kutaharibu maisha yao na taswira ya nchi kwa ujumla.
Akizungumza na wananchi wa Ngorongoro katika vijiji vya Kayapusi na Irkepus mhe. Lukuvi amesema wananchi hao wana wajibu wa kusimamia amani na utulivu katika eneo hilo na kuepuka ushawishi wowote wenye nia mbaya kutoka kwa watu wasiowatakia mema nchi yetu.
Waziri Lukuvi amesema wananchi wa tarafa ya Ngorongoro ni watanzania na wana haki sawa kama watanzania wengine, hivyo wana wajibu wa kusimamia maslahi ya nchi yao na kuepuka mbinu zozote zile zenye lengo la kuharibu Amani, utulivu, taswira ya nchi.
“Ndugu zangu kumbukeni kuwa ninyi ni sehemu ya watanzania, mna wajibu mkubwa wa kuhakikisha Ngorongoro inakuwa salama ili shughuli za utalii ziweze kuendelea na taifa liendelee kupata mapato kutoka kwa wageni wanaofika hapa,”alisema Waziri Lukuvi.
Waziri huyo ameongeza kuwa “Watalii hawa mnaoona wanaokuja kutembelea Ngorongoro ndio wanaotufanya tuwajengee miundombinu na huduma za kijamii, ndio wanaolipa mishahara watumishi wanaowahudumia, kwa hiyo nawaasa msirubuniwe na watu wa aina hii , mtakosa hifadhi, mtakosa huduma muhimu kama mtakubali kuingia kwenye mtego wao”, amefafanuaa Mhe Lukuvi.
Akizungumza katika mikutano hiyo Mkuu wa Mkoa wa Arusha mheshimiwa Paul Makonda amewashukuru wananchi hao kwa kuendelea kudumisha amani na utulivu na kusema kuwa hali hiyo imetoa heshima kubwa kwa mkoa huo na taifa kwa ujumla.
“Nawapongeza wananchi wa tarafa ya Ngorongoro kwa kuwa kudumisha Amani na utulivu hasa katika kipindi chote cha siku tano mlichokuwa na madai yenu, utulivu wenu ndio uliowezesha shughuli za utalii kuendelea bila changamoto yoyote katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro” amesisitiza Mhe. Makonda.
Wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro siku chache zizopita walikuwa wanaiomba serikali kufuta tangazo la kutokufanyika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji katika eneo hilo kwa maelezo kwamba zoezi la wananchi kuhama kutoka Ngorongoro kwenda Msomera na maeneo mengine ni la hiari.