Agosti 22, 2024 Mahakama ya Wilaya Ilala ilimtia hatiani mshtakiwa Sefania Adam Mwanja-ambaye ni Mweka Hazina wa Kikundi cha Afya Jamii.
Bw. Mwanja alikabiliwa na makosa ya Kughushi, Uhujumu Uchumi na Utakatishaji wa fedha haramu katika shauri la Uhujumu Uchumi namba 9069/2024 lililofunguliwa Aprili 8, 2024 mbele ya Mhe. Aneth Nyenyema-Hakimu Mkazi Mwandamizi.
Shauri hilo lilihusisha jumla ya washtakiwa wanne wote wakiwa ni wanachama wa kikundi hicho, ambapo: Mshtakiwa Bw. Mwanja yeye alikiri kutenda makosa hayo kwa utaratibu wa maridhiano na amelipa shilingi Milioni tano (Tsh.5,000,000/=), pamoja na kurejesha gari aina ya Toyota Premio yenye thamani ya Tsh 17,000,000.
Gari hili alinunua kwa fedha za mkopo wa shilingi milioni 100 na kulisajili kwa jina lake binafsi na hivyo ametakiwa kulirejesha kwenye umiliki wa kikundi.
Shauri hili lilitokana na udanganyifu uliofanywa na washtakiwa hao wanne kwa pamoja, ambao walijipatia mkopo wa shilingi Milioni Mia Moja (sh 100,000,000/=) kutoka Halmashauri ya Jiji la DSM na kuzitumia fedha hizo kinyume na matumizi yaliyokusudiwa.
Aidha, shauri dhidi ya washtakiwa watatu waliosalia ambao ni:
Erick Isack Gabriel, Sabina William Ndasi na Jacob Chacha Mwita litaendelea Septemba 18, 2024.