Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili leo Agosti 23, 2024 katika eneo la Pongwe Msungura, Msata Mkoani Pwani kwa ajili kufunga Zoezi la Medani katika Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali John Jacob Mkunda (kushoto) akipokea Bendera kutoka kwa Meja Jenerali Omary Nondo katika zoezi la kufunga Medani la Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yaliofanyikal eo Agosti 23, 2024 Pongwe Msunguru, Msata, Mkoani Pwani.
Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali John Jacob Mkunda leo Agosti 23, 2024 Pongwe Msunguru, Msata, Mkoani Pwani katika zoezi la Medani la Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) leo Agosti 23, 2024 Pongwe Msunguru, Msata, Mkoani Pwani katika zoezi la Medani la Maadhimisho ya Miaka 60 ya JWTZ.
Picha za matukio mbalimbali ya kufunga zoezi la Medani la Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yaliofanyika leo Agosti 23, 2024 Pongwe Msunguru, Msata, Mkoani Pwani. (Picha Noel Rukanuga)
………….
NA NOEL RUKANUGA, PWANI
Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameupongeza utendaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, huku akiwataka kuendelea kulinda misingi ya kuanzishwa kwa jeshi hilo pamoja na kudumisha nidhamu, utii, uaminifu na uhodari.
Akizungumza wakati akifunga zoezi la Medani la Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yaliofanyika leo Agosti 23, 2024 Pongwe Msunguru, Msata, Mkoani Pwani, Rais Dkt. Samia amesema kuwa kupitia mafunzo ya medani JWTZ wataendelea kuwa darasa kwa Afrika na Dunia kwa ujumla kutokana na uhodari waliokuwa nao.
Dkt. Samia amesema kuwa amefarijika baada ya kuona ubora wa Jeshi la JWTZ katika utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia nidhamu pamoja na uweledi.
“Askari anatakiwa kuwa na nidhamu, utii, uaminifu, uhodari na leo tumeshuhudia yalivyojitokeza kwa vitendo, nimefarijika sana, vijana wameonesha nidhamu ya hali ya juu, wametii maelekezo ya viongozi wao” amesema Dkt. Samia.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa mafunzo haya ni mazuri kwa ulinzi na usalama, huku akieleza kuwa ataendelea kutoa ushirikiano kwa JWTZ katika kuhakikisha jeshi linaendelea kuimarika na kufanya vizuri katika utekelezaji wa majukumu yake.
Amesema kuwa ataendelea kujenga Jeshi madhubuti lenye maafisa na askari wenye weledi pamoja na zana bora za kupambana na adui.
“Jeshi imara linatokana na dhamira ya kweli, moyo wa kujituma na uchumi imara, hivyo kadri tutakavyozidi kujenga uchumi ndivyo tutakavyozidi kuimarisha jeshi letu” amesema Rais Dkt. Samia.
Rais Dkt. Samia amelishukuru Jeshi la Jamhuri ya Watu wa China kwa kushiriki katika mazoezi ya pamoja na JWTZ ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 na ushirikiano uliopo, huku akifafanua kuwa ushiriki wao umefanikisha kubadilishana uzoefu ikiwemo kukabiliana na ugaidi, uvuvi haramu, usafirishaji wa watu na dawa za kulevya kwa kuzingatia matishio ya usalama.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali John Jacob Mkunda, amesema kuwa Jeshi limefanikiwa kutimiza majukumu yake ya msingi na ziada na kulijenga kuwa na uzalendo .
Jenerali Mkunda amesema kuwa wataendelea kusimamia misingi ya kuundwa kwa Jeshi ili kuendelea kuwa na jeshi bora linaloheshimika ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Amesema kuwa zoezi la medani limetumika kuona uwezo wa kipimo cha jeshi la JWTZ katika maeneo ya utimamu wa mwili, zana za kijeshi, kupima uwezo wa vikundi vya utawala kwa kuhudumia vikosi vinapokuwa mstari wa mbele kukabiliana na adui.
Jenerali Mkunda amesema kuwa katika maadhimisho ya miaka 60 ya JWTZ walianza na shamrashamra kwa kutoa huduma ya afya bure kwa wananchi ambapo Jeshi rafiki la Nchi ya China lilileta meli ya matibabu katika bandari ya Dar es Salaam na kutoa huduma kwa siku saba.
“Katika kuadhimisha miaka 60 ya JWTZ tulifanya mashindano ya michezo yajulikanayo CDF Gof, mazoezi ya ushirikiano kati ya JWTZ na jeshi la Ukombozi la watu wa China pamoja na mashindano ya utamaduni ya CDF yanayotarajiwa kuhitimishwa Agosti 30, 2024” amesema Jenerali Mkunda.
Jenerali Mkunda amesema kuwa lengo la mashindano ya utamaduni ni kukuza utamaduni wa Tanzania ikiwa ni sehemu ya kuunga juhudi za Rais Dkt. Samia katika kuona utamaduni wa mtanzania unalindwa kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Amebainisha kuwa JWTZ limejipanga kuendesha kampeni ya utoaji huduma ya afya bure itakayokwenda sambamba kwa wanajeshi kuchangia damu salama itakayoanza Agosti 28- 30, 2024.
Kilele cha Maadhimisho ya miaka 60 ya JWTZ kinatarajiwa kufanyika Septemba 1, 2024 katika uwanja Uhuru jijini Dar es Salaam ambapo kutakuwa na matukio mbalimbali ikiwemo Gwaride maalum, Uzinduzi wa kitabu cha miaka 60 ya jeshi la JWTZ, maonesho ya zana na vifaa mbalimbali vya jeshi.