Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akiwa kwenye kikao chake na Bodi/Menejimenti ya TANESCO kilichofanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akiwa kwenye kikao chake na Bodi/Menejimenti ya TANESCO kilichofanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto), Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga (katikati) na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka wakiwa kwenye kikao cha uongozi wa Wizara ya Nishati na Bodi na Menejimenti ya TANESCO kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya TANESCO, wakiwa kwenye kikao cha uongozi wa Wizara ya Nishati na Bodi hiyo pamoja na Menejimenti ya TANESCO kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga wakiwa kwenye kikao chao na Bodi na Menejimenti ya TANESCO kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
…………………………………………………….
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ameiagiza Bodi na Menejimenti ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha kuwa wanafanya tafiti kubaini vyanzo vipya vya uzalishaji umeme ili kuongeza kiasi cha nishati hiyo nchini na kuweza kufikia lengo la kuwa na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.
Dkt.Kalemani alitoa agizo hilo tarehe 19 Disemba, 2019 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kati ya Wizara ya Nishati na Bodi/Menejimenti ya TANESCO ambapo kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga.
“Lazima tufanye tafiti kubaini vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme ukiacha hivi vilivyopo, hata kama tusipotekeleza leo, vizazi vijavyo vitatekeleza miradi hiyo, mfano tafiti za mradi wa umeme wa Julius Nyerere (MW 2115) zilifanyika miaka mingi iliyopita, lakini mradi tunautekeleza sasa, hivyo nasi hatuna budi kuibua vyanzo vingine.” Alisema
Aidha, Dkt Kalemani aliiagiza Bodi na Menejimenti ya TANESCO kuhakikisha kuwa maeneo yote nchini yanaunganishwa na umeme wa Gridi ifikapo mwezi Juni 2022 ili wananchi wapate umeme wa uhakika na pia Serikali kuokoa fedha zinazotumika kununulia Mafuta ili kuendesha mitambo ya umeme kwenye baadhi ya maeneo nchini.
Kuhusu kazi ya usambazaji umeme vijijini, alisisitiza kuwa lengo la Serikali ni kufikisha umeme kwenye vijiji vyote ifikapo mwezi Juni mwaka 2021 na asilimia 85 ya wananchi wanapata umeme hivyo TANESCO ina jukumu la kuhakikisha kuwa lengo hilo linafanikiwa.
Vilevile, Dkt Kalemani aliiagiza TANESCO kuhakikisha kuwa, kila kiwanda au Taasisi ya umma inapojengwa, inafikishiwa umeme lengo likiwa ni kuongeza mapato ya Shirika na pia kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii nchini.
Aidha, aliiagiza Bodi na Menejimenti ya TANESCO kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Shirika kutoka shilingi Bilioni 46 zinazokusanywa sasa kwa wiki hadi kufikia Bilioni 52 kwa Wiki.
Dkt. Kalemani aliongeza kuwa, Shirika hilo pia linapaswa kumaliza madeni yake ifikapo mwaka 2026, linaboresha nidhamu ya watumishi ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi na kuhakikisha kunakuwa na mpango wa ukarabati wa miundombinu ya umeme kwenye maeneo yote nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, pamoja na kuipongeza TANESCO kwa majukumu mbalimbali wanayofanya, aliiagiza Bodi kujielekeza pia kwenye ukusanyaji wa madeni ya TANESCO kutoka kwa wateja mbalimbali zikiwemo Taasisi za umma kwani fedha zitakazopatikana zitasaidia Shirika kuweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Aidha, aliiagiza TANESCO kuangalia suala la malipo ya huduma ya umeme ili kuwe na utaratibu wa malipo hayo kufanyika kwa awamu ili kuweza kuunganishia umeme wananchi wengi zaidi na hivyo miradi hiyo ya umeme kuleta tija.
Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga, alisema kuwa, hali ya umeme nchini imeimarika hivyo TANESCO inapaswa kujikita pia kwenye kazi ya kuongeza wateja wa nishati hiyo ili kuongeza mapato.
Vilevile, alisisitiza kuhusu suala la mikoa yote nchini kuunganishwa na gridi ya Taifa ili kuimarisha hali ya umeme kwenye mikoa hiyo