**********************************
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo Disemba 19 ameweka jiwe la Msingi la ujenzi wa Jengo la Gorofa moja la Makao Makuu Chama cha mapinduzi Wilaya ya Kinondoni ikiwa ni Mkakati wake wa Kujenga ofisi nyingine Tano kama hizo kwenye Wilaya zote tano za Mkoa huo kwa lengo la kuhakikisha Viongozi wa Chama wanafanya kazi katika Mazingira bora na Mazuri.
Jengo hilo la Kisasa ndani yake litakuwa limesheheni Ofisi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Katibu Mwenezi, Kumbi tatu Kubwa zenye uwezo wa kubeba watu 230, Vyoo, Jiko, sehemu ya Kula, Stoo pamoja na ofisi za wenyeviti wa Jumuiya UVCCM, UWT na Umoja wa Wazee ambapo ujenzi wake unagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 2 ambapo ofisi hiyo inatarajiwa kukamilika na kuanza kutumika kabla ya Mwezi May Mwakani.
Aidha RC Makonda amesema kuwa ujenzi wa Ofisi hizo pia ni sehemu ya Mapenzi yake ya Dhati kwa Chama cha Mapinduzi CCM pamoja na kuunga mkono kazi nzuri na Bora inayofanywa na Mwenyekiti wa Chama hicho Rais Dkt. John Magufuli.
Pamoja na hayo RC Makonda amesema ili kuinua vijana katika vikundi vya hamasa ndani ya Chama hicho amepanga kuandaa mashindano ya vikundi hivyo kuanzia ngazi ya Wilaya na Mkoa na kikundi kitakachoshinda kitapatiwa Mtaji wa Shilingi Milioni 10 taslimu za kuanzisha miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake Mwenyekiti Wa CCM Mkoa wa Dar es salaam Mama Kate Kamba pamoja, Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es salaam pamoja na Viongozi wa CCM ngazi ya Wilaya wamempongeza RC Makonda kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM kupitia miradi mbalimbali anayoitekeleza kwa juhudi zake binafsi jambo linalosaidia kupunguza kero za wananchi.