Home Mchanganyiko MENEJIMENTI YA SEKTA YA UJENZI YARIDHISHWA NA MIRADI YA BARABARA MKOANI NJOMBE

MENEJIMENTI YA SEKTA YA UJENZI YARIDHISHWA NA MIRADI YA BARABARA MKOANI NJOMBE

0

Menejimenti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) wakipata maelezo kutoka kwa Mkandarasi wa Kampuni ya Cheon Kwang Engineering & Construction hatua za maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Lusitu – Mawengi yenye urefu wa kilometa 50, wakati wa ukaguzi wa miradi ya barabara inayoendelea
kutekelezwa mkoani Njombe.

Muonekano wa sehemu ya barabara ya Njombe – Moronga (km 53.9) inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Njombe. Ujenzi wa barabara hii unatarajiwa kukamilika
mwezi Januari, 2020.

Muonekano wa kazi za ujenzi wa sehemu ya barabara ya Lusitu – Mawengi (km 50) inayojengwa kwa kiwango cha zege la saruji zikiendelea, mkoani Njombe. Ujenzi wa
barabara hii unagharamiwa na Serikali kwa asilimia 100 na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2020.

******************************

Menejimenti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) imeridhishwa na hatua ya maendeleo ya miradi ya ujenzi wa barabara inayoendelea Mkoani Njombe mbali na changamoto mbalimbali ikiwemo ya mvua katika majira marefu ya mwaka.

 

Katika ziara hiyo Menejementi hiyo ilitembelea miradi mitatu ya barabara ambayo ni ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Njombe – Makete (km 107.4): sehemu ya Njombe – Moronga (km 53.9), Moronga – Makete (km 53.5) na ujenzi kwa kiwango cha zege la saruji barabara ya Itoni – Ludewa – Manda: sehemu ya Lusitu – Mawengi (km 50.0).

 

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Sekta hiyo, Bi. Ziana Mlawa, aliyekuwa akiongoza msafara huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi na kutembelea baadhi ya miradi inayotekelezwa Mkoani humo pamoja na kukagua
watumishi wa sekta hiyo walioko kwenye mafunzo kwa vitendo katika miradi hiyo.

 

Hata hivyo Bi. Mlawa alisema kuwa pamoja na kazi nzuri iliyofanyika, Sekta inaelewa changamoto hizo na kuwataka Wakandarasi hao kuongeza masaa ya kufanya kazi vipindi
ambavyo havina mvua ili kufidia muda uliopotezwa na kuwawezesha kukamilisha miradi
hiyo kulingana na mikataba.

 

“Wizara itajitahidi kuhakikisha mnalipwa fedha kwa wakati hivyo hakikisheni mnaongeza muda wa kufanya kazi ili kukabiliana na changamoto za mvua zilizopo katika ukanda huu” ameeleza Bi. Ziana.

 

Aidha aliwataka makandarasi wa miradi hiyo mbali ya kufanya kazi muda wa ziada wahakikishe wanaongeza vifaa vitakavyowawezesha kufanya kazi kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.

 

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, Kaimu Meneja Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Njombe Mhandisi Ruth Shalluah, amesema kuwa Wakala
umejipanga kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati, kusimamia mapungufu yanayochelewesha miradi na kuhakikisha yanatatuliwa kwa wakati.

 

Mhandisi Ruth ameeleza kuwa hadi sasa ujenzi wa barabara ya Njombe hadi Moronga umefikia asilimia 64 na barabara ya kutoka Moronga hadi Makete umefikia asilimia 46 pia ujenzi wa barabara ya Lusitu hadi Mawengi umefikia asilimia 42 na miradi yote inatekelezwa na fedha za serikali kwa asilimia 100.

 

Mkoa wa Njombe unahudumia jumla ya kilometa 1,153.74 kati ya hizo kilometa 403.98 ni barabara kuu na kilometa 749.760 ni barabara za mkoa ambapo hali ya mtandao wa
barabara hizo ni nzuri kwa asilimia zaidi ya 79.1.