Naibu Waziri Wizara ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mh.Deus Sangu akiongozana na Mkurugenzi Mkuu wa Watumishi Housing Investiment Dkt. Ferdy Msemwa wakati alipokagua nyumba za shirika hilo Magomeni jijini Dar es Salaam leo Agosti 19, 2024.
……………..
Shirika la Watumishi Housing Investment (WHI) limetakiwa kufuatilia mfuko wa mikopo kwa watumishi wa umma ambao upo chini ya Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya makazi ili kuuchukua na kuwa sehemu yao.
Rai hiyo imetolewa leo Jumatatu Agosti 19, 2024 na Naibu Waziri Wizara ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mh.Deus Sangu wakati alipotembelea Shirika hilo na kukagua nyumba zao Magomeni Jijini Dar es salaam.
“mfuko huo ni muhimu sana kwasababu watumishi wanapata changamoto nyingi sana hivyo kupitia Watumishi Housing Investment ndio suluhu ya matatizo ya watumishi na kwenye suala la makazi tukiwa na mifuko ambayo iko imara tutaenda kutatua matatizo ya watumishi”, amesema Sangu
Aidha, ameendelea kutoa msisitizo kwa shirika hilo kuweka utaratibu mzuri wa makusanyo ya fedha ambazo wanawakopesha watumishi nyumba kutokana na kuwepo kwa baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu kwenye ulipaji wa mikopo.
“Suala hili liko ndani ya Serikali kila mtumishi ambaye amekopeshwa nyumba ahakikishe analipa fedha ili zizidi kufanya kazi nyingine za ujenzi wa nyumba za watumishi”, amesema
Mwisho aliwaomba WHI waendelee kusimamia mfuko wa uwekezaji wa FAIDA FUND kisayansi na kitaalamu ili kuhakikisha wawekezaji wanakuwa na Imani hatua itakayosaidia kuwavutia wawekezaji wengi zaidi.
Kwaupande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Watumishi Housing Investment (WHI), Fredy Msemwa amesema wakati Shirika hilo linaanzishwa moja wapo ya malengo ilikuwa ni kwamba mfuko unaotumika kudhamini wakopaji wanaotoka katika sekta ya umma ambao uko chini ya Wizara ya Ardhi ulitakiwa kuhamishiwa hapa kwetu WHI
lakini juhudi ambazo tumezifanya bado hazikuwezesha mfuko huo kuhama kutokana na masuala ya kisera na kiuendeshaji ambayo yanafanya zoezi hilo lisiende kwa kasi.
“Moja wapo ni sehemu kubwa ya zile fedha zimekopeshwa kwahiyo utaratibu wa Jinsia ya kuuleta bado unafanyiwa kazi hivyo tunaomba tupate muda mzuri wakuendelea kuwasiliana na wenzetu wa Wizara ya ardhi ili ionekane njia ambayo itakuwa ya haraka zaidi katika kuwezesha suala hilo”, amesema Msemwa