Aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki Mkoani Arusha, Joshua Nasari (katikati) akizungumza na wageni wa China waliotembelea migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kushoto ni mchimbaji wa mgodi wa kampuni ya Flanoni, Aminiel Munuo.
……………………………………………………..
Aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki Mkoani Arusha, Joshua Nasari (Chadema) na wawekezaji 10 raia wa China wametembea migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara kwa lengo la kuwekeza.
Nasari na wageni hao wawekezaji 10 kutoka nchini China, walitembea machimbo hayo ya madini ya Tanzanite kwenye kitalu D.
Hata hivyo, aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki Joshua Nasari alisema hayupo tayari kuzungumza chochote juu ya ziara hiyo ya wawekezaji hao.
“Sitakuwa tayari kuzungumza juu ya hilo kwani hawa ni wageni kutoka China na wamefika kutembelea maeneo mbalimbali kwa lengo la kuwekeza hapa nchini,” alisema Nasari.
Mjiolojia wa Tume ya madini Mirerani, Selemani Hamis, ambaye aliongozana na wageni hao alisema wametembea migodi miwili ya madini ya Tanzanite iliyopo kitalu D.
Hamis alisema wametembea migodi miwili ya kampuni ya Flanoni na Edward Mollel ili kujionea shughuli za uchimbaji madini ya Tanzanite zinavyofanyika.
Alisema wao kama serikali wamewapa ushirikiano wa kutosha wageni hao ambao wametembea migodi hiyo ya Tanzanite na kujionea shughuli zinavyofanyika.
Mmoja kati ya wawekezaji hao Tao Xiangyang alisema kundi lao limehusisha wawekezaji wa sekta mbalimbali hivyo wametembea vivutio mbalimbali ili waweze kuwekeza.
Xiangyang amesema katika kundi hilo la wawekezaji 10 wapo wenye kuhitaji kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo madini, hoteli na ujenzi wa majengo makubwa.
Mfanyakazi wa mgodi wa kampuni ya Flanoni, Aminiel Munuo akizungumza na wawekezaji hao alisema wanafanya shughuli za uchimbaji madini kitaalamu kwa kutumia vifaa vya kisasa.
Munuo alisema wachimbaji madini ya Tanzanite hivi sasa wanatumia teknolojia ya kisasa ikiwemo mashine na siyo kama miaka iliyopita ambapo walikuwa wanazama migodini kwa kutumia kamba pekee.