Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Ndg. Philip Japhet Mangula akizungumza wakati alipokagua miradi mbalimbali ya maendeleo ya chuo cha mafunzo Ihemi mkoani Iringa leo Kushoto ni Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ali Kakurwa na kulia ni Mwenyekiti wa UVCCM Ndugu James Kheri.
Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ali Kakurwa akiweka jiwe la msingi katika moja ya majengo chuoni hapo.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Ndg. Philip Japhet Mangula akikata utepe wakati alipokagua miradi mbalimbali ya maendeleo ya chuo cha mafunzo Ihemi mkoani Iringa leo.
………………………………………………
Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Ndg. Philip Japhet Mangula akizungumza na wanaCCM mara baada ya kuzindua majengo na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ya chuo cha mafunzo Ihemi amewataka vijana kufuta fikra za kufikiria kuajiriwa badala yake wafikirie kujiajiri.
“Mnapokuja kwenye mafunzo hapa chuoni nataka mfute kabisa mawazo ya tunajifunza ili tukaajiriwe, hapa ni sehemu ya mafunzo ya kubadilisha fikra na mitizamo ya kwamba, kusoma ni kuajiriwa.” amesema Mzee
Mangula
Ameongeza kuwa vijana wabadili mitizamo ya kusoma ni kuajiriwa wengi wasome wakijua watajitegemea na chuoni hapo watafundishwa namna ya kujiajiri kwani ajira kubwa ni kilimo.
Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Bashiru Ally akizumgumza katika uzinduzi huo, ametangaza bodi ya muda ya ushauri wa chuo hiko itakayofanya kazi kuanzia sasa, ambapo wajumbe hao watakuwa katika bodi hiyo kwa nafasi zao.
Wajumbe wa bodi hiyo ni
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa (Mwenyekiti wa Bodi), Mkuu wa chuo (Katibu wa Bodi) na kwa sasa nafasi hiyo atakaimu Katibu wa Mkoa kwa kuwa uteuzi bado haujafanyika,
Mlezi wa mkoa wa Iringa ambaye kwa sasa ni
Ndg. Mizengo Peter Pinda,
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa,
Makatibu wa Jumuiya wa Mkoa
Mlezi wa jumuiya na
Idara ya Itikadi na Uenezi itateua mwakilishi mmoja, na kuongeza kuwa, bodi hii itakuwa chini ya Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM.
Kwa upande wake Mlezi wa CCM Mkoa wa Iringa Ndg. Mizengo Pinda amesema, moja ya malengo ya chuo hiko ni kujenga hisia ndani ya vijana juu ya siasa ya nchi hii kwa maslah ya watanzania.
Amesema kuwa, ni muhimu vijana kutambua uzalendo ni kitu gani hivyo yanapoanza mafunzo ni muhimu kujikita zaidi katika siasa na itikadi ili waweze kujua Taifa linataka nini na wao wajibu wao ni nini.
Kabla ya Mkutano huo, Ndg. Philip Mangula amezindua Kiwanda Cha ufundi stadi kushona kilicho chini ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na kukagua kilimo cha nyanya na mbogamboga chuoni hapo, wakati huo huo Katibu Mkuu ameweka jiwe la msingi wa ujenzi wa ukumbi chuoni hapo.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi na wanachama mbalimbali wakiongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu Maalim Juma Kombo, Mwenyekiti wa UVCCM na Mjumbe wa Kamati Kuu Ndg. Kheri James, Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Bi. Tabia Mwita, Katibu Mkuu wa UWT Mama Queen Mlozi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Ndg. Erasto Sima, Wajumbe wa Halmashauri Kuu, viongozi wa mila, viongozi wa dini, Wakuu wa Mikoa ya Iringa na Njombe, Mawaziri, Naibu Mawaziri, Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Iringa na Wabunge.