Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi akipatiwa maelezo na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Omar Said Shaabani wakati akiangalia Ramani katika hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi katika Mradi wa Eneo la Viwanda Dunga Zuze Wilaya ya Kati Unguja.





Na Sabiha Khamis Maelezo 07/08/2024
Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar inaendelea kuimarisha Sekta ya Viwanda ili kuleta maendeleo nchini.
Akizungumza katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi mtaa wa viwanda Dunga Zuze Mkoa wa Kusini Unguja, Waziri wa wizara hiyo Mhe. Omar Said Shaaban amesema Wizara inatekeleza miradi ya kuanzisha maeneo ya viwanda nchini.
Amesema Serikali katika kuhakikisha nchi inatoka katika kuagiza kila kitu kutoka nje ya nchi imeona ipo haja ya kuandaa miundombinu itakayowezesha kuzalisha bidhaa muhimu kwa matumizi ya wananchi kutoka ndani ya nchi.
Hatahivyo amemuomba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, chini ya kifungu cha 39 kifungu kidogo 2 cha Sheria ya uwekezaji ya mwaka 2023 kulitangaza eneo la mtaa wa viwanda Dunga zuze na Panga tupu kwa Unguja pamoja na Chamanangwe kwa Pemba kuwa ni eneo maalum la kiuchumi kwani Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda ndio wasimamizi wa maeneo hayo.
Akitoa taarifa ya kitalamu Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Fatma Mabrouk Khamis, amesema eneo hilo lina ukubwa wa ekari 173 ambapo kabla ya kuanza mradi huo Wizara imelipa fidia kwa vipando na majengo kwa wananchi wa eneo hilo.
“Jumla ya Shilingi 590, 743,815 kuwalipa fidia wananchi wa eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya mradi wa viwanda” alisema Katibu.
Amefafanua mradi huo umejumuisha ujenzi wa Tangi la maji lenye ujazo wa lita milioni 1, uchimbaji wa visima vitatu na usambazaji wa mabomba ili kurahisisha huduma wakati wa ujenzi.
Ameendelea kwa kusema kuwa mradi mwengine unaotekelezwa katika mtaa wa viwanda Dunga Zuze ni pamoja na ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 7.83 unaotekelezwa na Mkandarasi kutoka Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC).
Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2024 l/2025 imepanga kuendeleza mitaa yake viwanda jumla shilingi 40,320,000,000 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa ukuta mabanda ya viwanda, ujenzi wa miundombinu na umeme.
Jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa mtaa wa viwanda Dunga Zuze limewekwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi Tarehe 07/08/2024