NJOMBE,Wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akisaini Muswada wa Bima ya Afya kwa wote na kuwa sheria Wananchi mkoani Njombe wamesema ni muhimu zoezi la upatikanaji wa bima hizo likafanyika haraka kwani zina faida kubwa kutokana na uchumi wa sasa.
Aidha wananchi hao wamesema wamekuwa wakipata adha kubwa pindi wanapougua wakiwa hawana fedha na kujikutaka wanageuka kuwa omba omba kwa ndugu ili wapate matibu jambo ambalo wakiwa na bima ya afya watapata huduma bila usumbufu.
Baadhi ya wananchi hao akiwemo Ignas Lyimo na Hynes Mbaji wanakiri kuwa bima ya Afya ni muhimu kwani hawawezi kuwa na fedha wakati wote hivyo wakiwa nayo itawasaidia.
Kamishna wa Mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania TIRA Dokta Baghayo Saqware amesema mchakato wa kuanza kwa bima ya Afya kwa wote unaendelea na kinachosubiriwa ni kanuni za utekelezaji wa sheria ya bima Sura namba 394 kifungu kidogo cha 5.
Kwa upande wao Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Njombe Edward Mwakipesile amesema wapo tayari kuhamasisha wananchi na kuwapa elimu ya umuhimu wa bima ya afya hivyo mamlaka hiyo ijitahidi kuharakisha mchakato wa kanuni.
Sanjari na bima ya Afya kwa wote lakini Mamlaka hiyo imewataka watanzania kujiwekea utaratibu wa kukata bima hata za mali vikiwemo vyombo vya moto.