Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya DCEA inaendelea kuelimisha jamii juu ya tatizo la dawa za kulevya kwa lengo la kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa sahihi dhidi ya athari zinazotokana na matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya. Elimu hii inatolewa na maafisa wa Mamlaka waliofika katika Maadhimisho na Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa ya Nanenane yanayoendelea viwanja vya Nzuguni Dodoma.
Akizungumzana mbele ya waandishi wa habari waliotembelea banda la DCEA, Afisa Elimu Jamii Mwandamizi wa Mamlaka Ndg. Said Madadi amesema ushiriki wa Mamlaka kwenye maonesho ya Nanenane ni utekelezaji wa moja ya majukumu ya Mamlaka katika kutekeleza mkakati wa kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya (demand reduction) kwa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali kuhusiana na madhara ya matumizi ya dawa za kulevya pamoja na wakulima kuacha kujihusisha na Kilimo cha bangi na mirungi.
“Miongoni mwa madhara yanayopatikana kwa kulima bangi na mirungi ni kuondoa uoto wa asili.Bangi na mirungi hulimwa maeneo ambayo hayafikiki kirahisi na mara nyingi ni katikati ya misitu au milimani. Watu wanaolima mazao haya hukata miti na kuchoma misitu ili kupata mashamba kwa ajili ya kulima mazao hayo haramu”.
Ameongeza kuwa, maeneo yaliyokithiri kilimo cha bangi mirungi hawatilii mkazo kilimo cha mazao mengine halali kwa ajili ya chakula na biashara hivyo kuleta athari kwa Jamii husika na ameiomba jamii kuachana na shughuli hizo.
Hata hivyo, amebainisha athari za matumizi ya mirungi kuwa ni pamoja na kusababisha vidonda kwenye njia ya mfumo wa chakula, saratani, upungufu wa nguvu za kiume, kukosa usingizi na kusababisha usingizi mzito dawa inapoisha mwilini hivyo huweza kusababisha ajali kwa madereva na vifo visivyotarajiwa.
Kwa upande wa bangi amesema, mara nyingi watu wanaotumia dawa za kulevya huanza kwa kutumia bangi wakiwa katika umri mdgo hivyo kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kuathirika kiafya na kiakili.
“Mara nyingi watumiaji wa bangi huishia kutumia dawa nyingine za kulevya kama heroin na cocaine. Bangi inasababisha matatizo ya afya ya akili, ndio maana mtaani mtu akionekana anaokota makopo au matendo tofauti na matendo yanayotarajiwa kwa Jamii wanasema zile ni bangi”
Ameongeza kuwa, bangi ni moja ya dawa za kulevya yenye kemikali zaidi ya 400 lakini kemikali aina THC (Tetrahydrocannabinol) ndio inayoathiri ubongo. “Madhara ya bangi ni kuamsha magonjwa ya akili hususan anxiety, depression na phychosis. Pia huingilia utendaji kazi wa milango ya fahamu na kumfanya mtumiaji awe kwenye hali ya njozi ambapo ataona na kusikia vitu tofauti na uhalisia” amesisitiza Said
Naye Mfamasia Mwandamizi kutoka DCEA, Upendo Chenya amesema moja ya jukumu la Mamlaka ni kupunguza madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kupunguza uhitaji wa hizo dawa.
“Katika kupunguza madhara tunatoa tiba kwa waraibu ambapo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya serikali imekuwa ikiboresha huduma za tiba katika vituo vya afya ambapo kuna vitengo cha afya ya akili. Na sasa kuna vituo zaidi ya 16 nchini na vimeweza kusajili zaidi ya waraibu 17,000. Pia, kuna huduma za kisaikolojia ili kuweza kumsaidia mgonjwa na huduma zote hutolewa Bure” amesema Upendo.
Wadau mbalimbali wameendelea kutembelea banda la Mamlaka katika maonesho ya Nanenane ambapo kwa pamoja wamepata elimu sahihi juu ya tatizo la dawa za kulevya hususan madhara ya dawa za kulevya, kemikali bashirifu na udhibiti wake, Sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, huduma mbalimbali za tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya, ushauri na unasihi kwa waathirika wa dawa za kulevya pamoja na kuona aina mbalimbali za dawa za kulevya zinazodhibitiwa.