Na Mwandishi Wetu
PAMOJA na Tanzania kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 120, imeelezwa bado kuna changamoto ya lishe kwa jamii, ambapo takwimu za Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) 2020, zikionesha asilimia 34 ya watoto nchini wanaabiliwa na udumavu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Island of Peace (IDP) Tanzania, Ayesiga Buberwa wakati wa dhifa ya kitaifa ya chakula cha usiku cha asili iliyoandaliwa na shirika hilo na wadau wengine wa kilimo ikolojia nchini.
Alisema takwimu za WFP zinaonesha asilimia 34 ya watoto wenye miaka chini ya miaka mitano wanakabiliwa na udumavu, hivyo kama kuna mambo ya kuangalia kwa umakini kwa sasa ni kuhusu afya ya watu.
Ayesiga alisema anavyosema asilimia 34 ya watoto ni sawa na kusema kati ya watoto 100 watoto 34 wana utapiamlo wa udumavu na kwamba udumavu huo hauhusu mahindi wala wanyama, bali ni mustakabali wa watu.
Mkurugenzi huyo alisema taarifa hiyo ya WFP ilisema pia asilimia 62 ya vijana wenye miaka 15 hadi 18 wana udumavu, hivyo ni wazi kuwa udumavu ni changamoto kubwa nchini.
“Takwimu zinaonesha Tanzania inajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 120, jambo ambalo ni la kupongezwa, ila kuna changamoto kubwa ya udumavu wa watoto wetu na rika la kati, tunapaswa kukabiliana nayo kwa pamoja kwa kusisitiza ulaji wa vyakula vya asili,” alisema.
Alisema kuna jitihada zinachukuliwa na wadau mbalimbali katika kukabiliana na changamoto hiyo, ila ameomba nguvu kubwa kuongezeka hasa katika kuhamasisha ulaji wa vyakula asili ambayo utafiti utafiti umeonesha vina faida.
“Sijasema changamoto za ukosefu wa damu na madini kwa mama wajawazito na wanaonyonyesha, vyote hivyo ukiviangalia, ikiwemo njaa iliyofichika, udumavu na utapiamlo, vyote hivyo vinasababishwa na nini tunakula, tunakula saa ngapi, kwa namna gani na kuviandaa aje,” alisema.
Ayesiga alisema changamoto nyingine ya kula vyakula visivyo vya asili ni uzito uliokithiri kuongezeka.
Mkurugenzi mkazi huyo alisema changamoto hizo zinapaswa kuwafikirisha viongozi wa hali ya juu, ili kuhakikisha tatizo hilo linapunguzwa, iwe kwa kutunga sera au kufanya utafiti wa kina kupitia taasisi za kitafiti kama Kituo cha Utafiti Tanzania (TARI), Chuo Kikuu cha Nelson Mandela na wengine.
Alisema iwapo kila mdau atafanyia kazi eneo lake kwa kina, upo uwezekano wa kuifanya jamii ifurahie chakula cha asili na kuondoa changamoto ya njaa iliyofichika.
“Vyakula vya asili vinalenga kutunza utamaduni wetu, hivyo sisi kama Islands of Peace tunajitahi kwa upande wetu kuikomboa jamii ya kitanzani katika eneo la lishe,” alisema
Ayesiga alisema katika dhifa hiyo ambayo imebeba na kauli mbiu ya ‘Kuboresha Lishe kupitia Vyakula Asili na Kitamaduni’ wameshirikiana kuanda na Wizara ya Kilimo, Pelum-Tanzania, Shirikisho la Vyama vya Wakulima na Wafugaji Tanzania (SHIWAKUTA) na We Effect.
Akizungumza katika hafka hiyo Mgeni rasmi Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amezitaka tasisi zinazohamasisha kilimo ikolojia hai kushirikisha viongozi wa dini, serikali na shule ili uelewa uweze kufikia watu wengi.
“Mimi nimetafakari sana namna ya kukabiliana na changamoto hii ya udumavu ambayo imetajwa napenda kutumia nafasi hii kuziomba taasisi zote za kupigania kilimo ikolojia hai weweke mkazo kwa viongozi wa dini, serikali za mitaa na shuleni, tutaweza kugusa jamii kubwa,” alisema.
Alisema watendaji wa serikali wana nafasi kubwa ya kusaidia jamii kuondokana na udumavu, kwani kwa hali ilivyo sasa mtu anayekula mbogamboga anaonekana hana akili, kumbe wasio kula ndi wana tatizo.
Waziri mkuu huyo mstaafu alisema ni vema Wizara ya Kilimo, Afya, Fedha na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikal za Mitaa (TAMISEMI), ziweze kukutana na kujadiliana namna ya kukabiliana na changamoto ya udumavu na kueleza nini cha kufanya kwa maslahi ya nchi.
Pinda alisema nchi ya Tanzania ambayo ina ardhi nzuri, mvua za kutosha ni aibu kuwa na zaidi ya watoto milioni 3.4 kuwa na udumavu, hivyo ni lazima viongozi wote hasa wenye uwezo kuchukua hatua ili kuokoa taifa hili.
“Inawezekana watendaji wanatuangusha, ila sisi viongozi ambao tumebahatika kuwa na maisha bora tumesababisha hali hii, ni wakati wa kubadilika na kuiambia jamii faida ya kula mbogamboga kwa mwanadamu,” alisema.
Waziri mkuu huyo mstaafu alisema hakuna sababu ya Tanzania kutamba kuwa katika uchumi wa kati wakati watu wake ni wadumavu.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema uamuzi wa IDP kuandaa dhifa hiyo ya chakula asili unapaswa kuungwa mkono kwa kuwa unaenda kukomboa wananchi.
Alisema serikali inatambua kazi kubwa ambayo inafanywa na taasisi zinazopigania kilimo ikolojia na ndio maana katika bajeti wametenga fedha za ruzuku katika eneo hilo na ameahidi wataendelea kukiunga mkono kilimo hicho.
“Tumejipanga kuendelea kilimo ikolojia hai ili kiwe na tija, kama kilivyo kilimo kingine, kwani ushihidi unaonesha kina faida kiafya na kiuchumi,” alisema.
Alisema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetenga fedha nyingi kwenye kilimo, hali ambayo imesababisha sekta hiyo kuwa ya tatu kwa kuchangia fedha za kigeni.