Meneja wa Tarura mkoa wa Ruvuma Mhandisi Silvester Chinengo kushoto akikabidhi mkataba wa miradi ya ujenzi wa barabara Mkandarasi wa Kampuni ya Kimango Engneering Co Ltd Happy Kimaro wakati wa hafla ya utiaji saini Mikataba ya matengenezo ya barabara za mkoa wa Ruvuma kwa mwaka wa fedha 2024/2025 iliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma.
Baadhi ya wakandarasi wakimsikiliza Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Ahmed Abbas(hayupo pichani),wakati wa hafla ya utiaji saini Mikataba ya matengenezo ya barabara za mkoa wa Ruvuma kwa mwaka wa fedha 2024/2025 iliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma.
Picha no 352 Meneja wa wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA Mkoani Ruvuma Mhandisi Silvester Chinengo,akitoa taarifa ya mapokeo ya fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara zilizo chini ya TARURA kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Ovans Contructions Co Ltd Vales Urio,akizungumza kwa niaba ya wakandarasi wa mkoa wa Ruvuma wakati wa utiaji saini wa mikataba ya matengenezo kwa baadhi ya barabara za mkoa wa Ruvuma zilizo chini ya usimamizi wa wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas,akizungumza na watumishi wa Tarura,Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali katika mkoa huo(hawapo pichani) wakati wa utiaji saini wa mikataba ya matengenezo ya barabara zinazosimamiwa na TARURA mkoani humo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Baadhi ya wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali mkoani Ruvuma,wakimsikiliza Mkuu wa mkoa huo Kanali Ahmed Abbas,wakati wa hafla fupi ya utiaji saini wa mikataba ya matengenezo ya barabara zinazosimamiwa na TARURA mkoani humo.
……………..
Na Mwandishi Maalum, Songea
WAKALA wa barabara za mijini na vijijini(Tarura)mkoa wa Ruvuma,kwa mwaka wa fedha 2024/2025 umeidhinishiwa katumia kiasi cha Sh.bilioni 22,194,409,504.77 kwa ajili ya kufanya matenengezo ya barabara zake.
Meneja wa Tarura Mhandisi Silvester Chinengo alisema,kati ya fedha hizo kutoka Mfuko Mkuu wa Barabara ni Sh.bilioni 7,894,961,998.36 na mfuko mkuu wa Serikali(kila jimbo)Sh.bilioni 4,500,000,000.00 na fedha za tozo ya mafuta Sh.100 kwa lita Sh.bilioni 9,799,447,506.41.
Chinengo amesema hayo leo,kwenye hafla fupi ya utiaji saini mikataba ya matengenezo ya Barabara iliyofanyika katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma mjini Songea.
“Mpaka sasa Tarura tumekamilisha manunuzi ya miradi hamsini yenye gharama ya Sh.bilioni 14,19,607,702.00 ambapo jumla ya kilometa 1,079 za barabara zitafanyiwa matengenezo ya aina mbalimbali pamoja na ujenzi wa makalavati na madaraja”alisema Chinengo.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Ahmed Abbas alisema,serikali kupitia Tarura itahakikisha inawalipa Wakandarasi fedha zao ili kuwajengea uwezo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Ameziagiza Taasisi za serikali mkoani humo,kulipa madeni yao ili kuwaepusha wakandarasi kuingia kwenye migogoro mbalimbali ikiwemo kunyang’anywa na kuuzwa mali zao na taasisi za fedha kutokana na fedha walizokopa kama mitaji katika shughuli zao.
Alisema,serikali kupitia sekta ya mawasiliano ya barabara imejipanga kuona sekta ya barabara inaimarika ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao kutoka shambani kwenda mijini kwa ajili ya kupata soko la uhakika.
Katika hatua nyingine Abbas,amezitaka Taasisi za Serikali mkoani humo, kuwapa kipaumbele wakandarasi wazawa na kutoa upendeleo kwa wanawake wanaofanya kazi za ukandarasi ili kuwajengea uwezo na waweze kunufaika na fedha zinazoletwa katika mkoa huo kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Aidha,amewapongeza watumishi wa Tarura wilaya na mkoa wa Ruvuma kwa kazi nzuri wanazozifanya za kuunganisha mawasiliano ya barabara kati ya wilaya moja na nyingine na mkoa wa Ruvuma na mikoa mbalimbali hapa nchini.
Mkuu huyo wa mkoa,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa uwezeshaji wake mkubwa katika sekta ya mawasiliano yaliyosaidia mkoa huo kuwa na mawasiliano ya uhakika katika kipindi chote cha mwaka.
Ametoa wito kwa wakandarasi wanaofanya kazi mkoani Ruvuma, kuwa na utaratibu wa kujitambulisha kwa viongozi wa serikali ngazi ya wilaya na mkoa ili wafahamike na kupata ushirikiano wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Mary Makondo,amewataka watendaji wa Tarura kuwafuatilia kwa karibu wakandarasi ili miradi inayotekelezwa ikamilike kwa muda uliopangwa na kwa viwango vinavyohitajika.
“Wakandarasi fanyeni kazi zenu kulingana na makubaliano yaliyopo kwenye mikataba,nendeni mkatekeleze miradi kwa viwango na kuzingatia muda uliopangwa na siyo vinginevyo”alisema.
Naye Mkuu wa Takukuru mkoani Ruvuma Hamza Mwenda alisema, Takukuru itahakikisha inafuatilia miradi yote iliyopangwa kutekelezwa ili kujiridhisha ubora wa miradi husika.
Alisema,fedha hizo zinalenga kurahisisha na kuboresha maisha ya wakazi wa mkoa wa Ruvuma,hivyo wakandarasi wana wajibu wa kuonyesha uaminifu na uadilifu kwa serikali kwa kutekeleza miradi yenye viwango.
“Takukuru tumejipanga kuhakikisha miradi yote itakayotekelezwa na fedha hizi inakuwa na viwango ili wananchi wajivunie na kunufaika naSerikali yao ya awamu ya sita,hatutosisita kukufikisha Mahakamani pale tutakapokuta mradi uliotekeleza uko chini ya viwango”alisema Mwenda.
Mwakilishi wa Wakandarasi wa mkoa wa Ruvuma Vales Urio kutoka kampuni ya Ovans Contructions Ltd,ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwaamini na kuwapa kazi za ujenzi wa miradi ya barabara na kuhaidi watekeleza miradi hiyo kwa ubora ili kuleta tija kwa mkoa na Taifa.