Na. WAF – Morogoro
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekitaka kiwanda cha Sigara cha Serengeti (SCC) pamoja na viwanda vingine nchini kuunga Mkono juhudi za Serikali katika kusaidia Mfuko wa Bima ya Afya kwa wote.
Rais Samia amesema hayo leo Agosti 6, 2024 wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha ‘Serengeti Cigarette Company’ (SCC) na upanuzi wa kiwanda cha uchakataji tumbaku (MTPL) wakati wa ziara yake mkoani Morogoro.
“Mtusaidie katika Bima ya Afya ili wale watakaokuja na vifua wana kohoa wapate matibabu kwa urahisi bila kikwazo cha fedha, naomba mtuunge mkono katika hilo.” Amesema Rais Dkt. Samia
Rais Samia ameuhakikishia uongozi wa kiwanda hicho cha ‘Serengeti Cigarette Company’ (SCC) kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono ili Watanzania waweze kupata kunufaika na uwekezaji huo.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ziara yake mkoani Morogoro ameambatana na viongozi wa Serikali wakiwemo Mawaziri kutoka Sekta mbalimbali akiwemo Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu.