Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda ni kati ya Washiriki wa Maonesho ya Wakulima Maarufu kama Nane Nane katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Katika Maonesho hayo ,TIRDO inatoa elimu juu ya Uzalishaji wa Mafuta Tete(Essential Oil) ,Uongezaji wa thamani katika mazao ya kilimo ,Matumizi bora ya Nishati Viwandani na Majumbani( Energy Effeciency) pamoja na uzalishaji wa nishati safi kwa mazingira (Clean Cooking Energy )
Mtaalam wa Uongezaji wa thamani mazao Mwandamizi Bi.Jaqueline Mwendwa anasema watembeleaji wengi wamevutiwa na uzalishaji wa mkaa mbadala unaotokana na Pumba na Mabaki ya mbao ( Maranda).
“Unajua pumba ni changamoto katika maeneo mengi nchini na ni mojawapo wa uchafuzi wa Mazingira ,hivyo mtu anapopata njia rahisi ya kuziondoa na kuongeza kupata bidhaa mbadala inakuwa ni suluhu kubwa kwa jamii” aliongeza Bi.Mwendwa.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Biashara katika Wizara ya Viwanda na Biashara ndugu Sempeho Manongi Nyari pamoja Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) ndugu William Erio ni kati ya watembeleaji wa banda la TIRDO ambapo wamefurahia teknolojia zilizowasilishwa na TIRDO.
Ndugu Sempeho alihimiza teknolojia zinazovumbuliwa na watafiti kufika kwa wananchi .
“Nimefurahi kuona maganda ya Machungwa yanaweza kuzalisha mafuta lakini ni wakati hii teknolojia ifike kwa wananchi” aliongeza ndugu Sempeho.
Maonesho hayo yalianza tarehe moja Agosti na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe nane Agosti 2024.