Meneja Uendeshaji Bodi ya Bima ya Amana DIB Bw. Nkanwa Magina akitoa elimubya usalama wa fedha kwa mmoja wa wananchi waliotembelea banda la DIB katika maonesho ya Nanenane viwanja vya Nzuguni Dodoma leo Agosti 5,2024.
……………….
Meneja Uendeshaji Bodi ya Bima ya Amana DIB Bw. Nkanwa Magina amesema DIB Ilianzishwa kwa sheria ya benki na taasisi za fedha ya mwaka 1991 ambayo ilihuishwa mwaka 2006 na kukasimiwa Majukumu inayoyatekeleza.
Majukumu yake makubwa ni kusimamia mfuko wa bima ya amana ambao unachangiwa na benki zote zilizopewa leseni na benki kuu (BoT) ya kufanya biashara ya kibenki hivyo benki zote zinatakiwa kuchangia katika mfuko huo.
Amesema pale benki inapofungwa na benki Kuu BoT na kuwekwa chini ya ufilisi jukumu la bodi ya bima ya amana ni kulipa fidia ya bima ya amana ili wateja waliokuwa wanahudumiwa na benki hiyo wasipoteze pesa zao.
Ameongeza kuwa kwa sasa kiwango cha juu cha fidia ya bima ya amana kwa wateja wa benki yoyote ambayo ina leseni ya benki kuu pale itakapofungwa na kufilisiwa ni kuanzia shilingi moja mpaka milion 7.5 ambapo awali ilikuwa ni shilingi moja mpaka milioni 1.5 na kwa kiwango hicho tunafikia asililia 99 ya wateja wa benki na taasisi za fedha hapa nchini.
Mara nyingi katika kumteua Mfilisi wa benki inategemeana na BOT itamteua nani kuwa mfilisi lakini kwa unyeti wa biashara ya kibenki mara nyingi kisheria BoT inamteua bodi ya bima ya amana kama mfilisi kutokana na unyeti wa biashara yenyewe ambapo kwa sasa wamefilisi benki 9 za zamani na hatua mbalimbali zinaendelea na zimefikia pazuri.
Awali DIB ilikuwa inashiriki kwenye maonesho yote ikiwa ndani ya banda la benki kuu lakini kwa sasa imeshiriki kutoa huduma yenyewe ambapo tangu kuanza kwa maonesho haya hapa Dodoma wananchi wamefurahishwa kutokana na elimu waliyoipata katika maonesho hayo kuelewa huduma zinazofanywa benki na kujua kuwa pesa zao walizoweka kama amana zipo salama hata kama benki ikifa wanaweza kufidiwa
DIB imeshauri taasisi nyingine kama Saccoss na Vikoba nazo ziwe na mpango wa bima ya amana ili kuwepo na usalama wa fedha za wananchi wanaopata huduma za kifedha katika taasisi hizo.