Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni Elizabeth Mokiwa akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 5, 2024, Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utendaji katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia April hadi June, 2024.
……..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imefanikiwa kufatilia utekelezaji wa miradi sita yenye thamani ya Sh. 8,056,860,672.6 ambayo inaendelea na utekelezaji, huku wakibaini mapungufu machache ambapo wahusika wameshauriwa kurekebisha pamoja na kufatiliwa kwa ukaribu ili kuhakikisha inakamilika kwa ubora na kuzingatia thamani halisi ya fedha.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 5, 2024, Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utendaji katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia April hadi June, 2024 Naibu Mkuu wa TAKUKURU Kinondoni, Elizabeth Mokiwa, amesema kuwa miongoni mwa miradi iliyofatiliwa ni mradi wa ufungaji wa Pampu ya maji uliopo Kibamba Kisarawe katika Manispaa ya Ubungo wenye thamani ya Sh. 569, 000, 000.
“Mradi huu ulikuwa umekamilika na upo katika kipindi cha majaribio, changamoto tuliobaini pampu mpya iliyofungwa ilikuwa inavuja maji hivyo kuathiri ubora wa mradi, na Mkurugenzi wa DAWASA aliandikiwa barua ili kutatua kero hiyo iliyobainika wakati wa ufatiliaji” amesema Mokiwa.
Mokiwa amesema kuwa pia wamefanikiwa kufanya kikao na wadau wa ukataji na uwasilishaji wa Kodi ya zuio katika ununuzi wa vifaa na huduma katika Manispaa ya Kinondoni ambapo wananchi wamenufaika na elimu ya matumizi ya mashine za EFD na kiwango sahihi cha kodi kinachostahili kukatwa.
“Elimu hii inaendelea kutolewa na kodi inakatwa na kuwasilishwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa wakati kama walivyokubaliana katika kikao hicho” amesema Mokiwa.
Mokiwa amesema kuwa wanaendelea kutoa tahadharisha kuhusu vitendo vya rushwa kipindi hasa kipindi hiki Taifa linapojiandaa na uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu.
Amesisitiza rushwa katika uchaguzi husababisha kuchaguliwa kwa viongozi wasio waadilifu, watakaotumia muda wao mwingi kurejesha fedha walizotumia na si kuleta maendeleo kwa wananchi, huku akieleza kuwa wananchi wanapaswa kushirikiana na taasisi hiyo kutokomeza vitendo hivyo.
“Takukuru tunadhibiti rushwa wakati wote, ingawa kipindi hiki nchi inapoelekea kwenye uchaguzi tumeweka msisitizo mkubwa kwa sababu tunafahamu athari zake” amesema na kuongeza;
“Kiongozi atakayechaguliwa kwa kutoa rushwa hawezi kuwa mwadilifu, atatumia muda mwingi kurejesha fedha alizotumia na si kuleta maendeleo kwa wananchi.”
Mokiwa amesema katika kukabiliana na vitendo hivyo wameanza kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya rushwa wakati wa uchaguzi na wananchi wanapaswa kushirikiana na taasisi hiyo kuvitokomeza kuanzia sasa, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.
“Tunaendelea kupokea malalamiko yanayohusu rushwa na kuyafanyia kazi kwa haraka, ili kudhibiti vitendo hivyo,” amesema.
Amesema pia wanatoa elimu ya rushwa shuleni na vyuoni, kufanya vikao na wadau na kuwaelimisha wananchi kuhusu madhara ya rushwa.
Katika hatua nyengine amesema kuwa wamepokea malalamiko 88 na kati ya hayo 32 yakihusu rushwa na yameshughulikiwa, sasa yapo katika hatua mbalimbali.