Mkurugenzi wa Kitengo Cha Mawasiliano na Masoko chuo kikuu Cha Dodoma Rose Joseph ameeleza kuwa Chuo hicho kinafanya utafiti wa mazao ya kilimo yanayoweza kulimwa katika kipindi Cha ukame katika Mkoa huo na kuwa na uzalishaji mkubwa.
Hayo ameyabainisha Agosti 3, 2024 katika maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya Nzuguni Mkoani Dodoma.
Amesema kuwa katika maonesho hayo ya kilimo chuo hicho kimeweza kuwa na kitalu ambacho wanalima mazao ambayo hawaweki viwatilifu wala kupiga dawa.
“Mfano tumekuja na nyanya pamoja na matango na ukiangalia matango ni makubwa sana tofauti na ambavyo tumezoea kwenye masoko, na hii inaonesha namna gani tunatumia utaalam wetu wa kisayansi katika kulima” Amesema Rose.
Rose ameeleza kuwa wakitengeneza mifumo ambayo itasaidia kuwa na kilimo bora wadau watavutiwa na kujitokeza katika uwekezaji na kupata suruhisho litakalosaidia kufikia uzalishaji mkubwa Kwa kutumia teknolojia na Kwa njia rahisi.
“Sisi tuna mifumo ambayo wanafunzi wetu wanayoitumia Kwa kutumia teknolojia inayorahisisha katika swala la kilimo” Amesema Rose.
Kwa upande mwingine ameeleza kuwa katika maonesho hayo wametumia fursa ya kukutana na wadau mbalimbali wakiwemo wa kilimo ili kuonesha vitu vinavyofanywa na chuo hicho kikuu Cha Dodoma.
Aidha Rose ameeleza kuwa wamekuja na bidhaa mbalimbali zinazomilikiwa na wanafunzi mwenyewe lengo likiwa ni kuwaandaa wanapohitimu masomo yao waweze kujitegemea wenyewe.
” Kwa mfano utaweza kuona chuo chetu kimekuja na Mvinyo (Wine) zinazotokana na mazao ya nyuki yaani asali inayozalishwa na chuo kikuu Cha Dodoma ” Amesema Rose