Na. Brigitha Kimario – Saanane/Mwanza
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasilia na Utalii anayeshughulikia Utalii – Nkoba Mabula amewahimiza na kuwasisitiza wakazi wa jiji la Mwanza kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta inayokua kwa kasi ya utalii ili kuendana na mahitaji ya watalii wanaoongezeka nchini kila mwaka.
Kauli hiyo aliitoa Julai 31, 2024 katika Chuo cha Wanyamapori Pasiansi alipokuwa akihitimisha ziara yake na kuziagiza taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kutoa elimu na kuhamasisha wadau mbalimbali kuzitambua fursa za uwekezaji ili wananchi wawekeze na kujipatia mapato.
Akiwa katika ziara hiyo Mabula alisema, “Ongezeni bidii na mbinu mbalimbali kutangaza utalii katika maonesho, mikutano ya kitaifa na kimataifa na pia shirikianeni na wadau wa usafirishaji na wenye makampuni ya utalii ili tupate watalii wengi zaidi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.”
Aidha, Mabula alieleza kuwa mawakala wa utalii kutoka Kaskazini mwa Tanzania wana uzoefu mkubwa kwenye masuala ya utalii hivyo wahamasisheni wawekeze jijini Mwanza ili kuwe na miundombinu rafiki ya kuwezesha watalii wanaozuru Kaskazini na Serengeti waje pia na Hifadhi zilizopo Kanda ya Ziwa.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara Massana Mwishawa alisema, “TANAPA imeendelea kuimarisha miundombinu ya malazi na kuanzisha mazao mapya ya utalii katika Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane. Lengo la kufanya hivyo ni kuongeza mapato kwa Taifa na hifadhi pia ili iweze kujiendesha kimapato.”aliongeza Kamishna huyo.
Kamishna Mwishawa alisema kuwa upatikanaji wa malazi na mazao mapya tunayoendelea kuongeza ndani ya Hifadhi hii yataongeza mapato na kuchangia uchumi wa nchi.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi – Tutindaga George Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane alisema, “Hifadhi imejenga mahema kwa ajili ya malazi kwa watalii watakaotembelea hifadhi hii ili wanaotaka kulala wasikose fursa hiyo kama ilivyokuwa awali.
Shirika linaendelea na jitihada za kuweka samani katika mahema hayo yaendane na hadhi ya kimataifa ili kuwawezesha watalii kufurahia thamani ya fedha zao walizowekeza katika safari yao ndani ya hifadhi hii pekee iliyopo katikati ya jiji la Mwanza.