Mkurugenzi wa Kinga, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi akieleza jambo mbele ya Maafisa Afya wa Mikoa na Halmashauri, wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya usafi wa mazingira.
Afisa kutoka Idara ya Mazingira Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee naWatoto Bw. Anyitike Mwakitalima akieleza mafanikio mbali mbali yaliyopatikana kutokana na afua mbali mbali za usafi wa mazingira zinazotekelezwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau.
Maafisa Afya kutoka Mikoa, Halmashauri na Wadau wakifuatilia kwa makini neno kutoka kwa Mkurugenzi wa Kinga, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi.
*********************************
Na. Catherine Sungura,Dodoma
Maofisa afya wa mikoa na halmashauri wametakiwa kusimamia afya ya jamii kwenye maeneo yao ili wananchi wajikinge dhidi ya magonjwa yakuambukiza na yele yasiyoambukiza.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa kinga Dkt. Leonard Subi wakati akiongea na maofisa hao ambao wanakutana jijini hapa kwa kikao kazi cha siku tatu wakijadili utekelezaji wa maazimio yaliyotolewa kwenye mkutano mkuu wa kwanza mwaka jana na Waziri Mkuu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.
“Mkutano huu ni wa pili mwaka huu,ni mkutano muhimu kwa maofisa afya kwani ndio wasimamizi wa shughuli za afya katika ngazi za jamii kwa kuhakikisha wananchi wanajikinga na maradhi, kula chakula bora kuishi makazi bora,usafi wa mazingira pamoja na kuwa vyoo bora”.Amesema Dkt. Subi
Aidha, amesema katika mkutano huu mambo mbali mbali yatajadiliwa ikiwemo afya mazingira,usafi na uchafuzi wa mazingira na kila kinachotumiwa na kumzunguka mwananchi ,pia wataangalia mabadiliko ya tabia nchi na kupata taarifa kutoka ngazi za mikoa ni jinsi gani walivyotekeleza majukumu yao.
“Maafisa afya muendelee kuishauri wizara kwa kutumia takwimu kwani tunatarajia mkutano huu mtabadilishana uzoefu kutoka sehemu zenu za kazi,kama wizara tumekua tukitengeneza sera na miongozo mbali mbali ya kudhibiti maradhi yote yanayoweza kuathiri afya za binadamu hivyo kazi ya wizara ni kukusanya taarifa,kuchakata na kuzitolea miongozo na maelekezo”. Aliongeza Dkt. Subi.
Hata hivyo amesema maofisa hao wana majukumu ya kusimamia na kulinda afya mipakani ili kusiingie magonjwa ya milipuko kutoka nje hususan nchi za jirani pamoja na utoaji wa chanjo ambapo Tanzania ipo vizuri.
Mkutano huo ambao utafunguliwa kesho na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu umebeba Kauli mbiu isemayo “Huduma bora za afya mazingira na usafi ni kichocheo muhimu cha uchumi endelevu.