Home Mchanganyiko MIAKA 4 YA JPM, MILIONI 500 ZATUMIKA KUBORESHA SEKTA YA MAJI-DKT. MANEGE

MIAKA 4 YA JPM, MILIONI 500 ZATUMIKA KUBORESHA SEKTA YA MAJI-DKT. MANEGE

0

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Nchini(WMA), Dkt. Ludovick Manege akizungumza Katika Mkutano wake na Waandishi wa Habari (Hawapo Pichani), Kuhusu mafanikio ya WMA katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Idara ya Habari- MAELEZO, Jijini Dar es Salaam leo Disemba 16, 2019.

*******************************

Na.Mwandishi Wetu-MAELEZO

16.12.2019

Serikali ilitoa kiasi cha shilingi milioni 500 kwa Wakala wa Vipimo Nchini (WMA) ili kuiwezesha wakala hiyo kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kuleta usawa katika biashara baina ya wateja na wauzaji hasa kwenye sekta ya maji.

 

Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo, Dkt.Ludovick Manege, alisema kuwa wakala unatekeleza
Sera ya Awamu ya Tano, kuhusu ujenzi wa viwanda na uchumi wa kati ambapo Rais John Pombe Magufuli alitoa TZS milioni 500 ili kuleta ufanisi katika wakala hiyo.

 

“Serikali iliipatia WMA shilingi milioni 500 ambazo zimeweza kununua vigezi vya kisasa gredi ya pili vinavyotumika kuhakiki mizani ya madini hivyo kuiwezesha Serikali kupata mapato yanayostahili kupitia vipimo sahihi kwenye sekta mbalimbali za kiuchumi”, Alisema Dkt.Manege.

 

Katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, WMA imeweza kujenga kituo kipya cha kisasa cha upimaji wa malori ya mafuta kilichopo Misugusugu Mkoani Pwani ambacho kinapima malori 400 kwa mwezi na kuingiza kiasi cha shilingi milioni 300 kila mwezi, na hivyo kuifanya Serikali kukusanya mapato stahiki
kwenye sekta ya usafirishaji mafuta.

 

Dkt. Manege alisema kuwa WMA imeboresha sekta ya maji baada ya kuwepo kwa vipimo ambavyo vinaleta usahihi kwa matumizi ya dira za maji na mpaka sasa WMA
imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi kwa kuwezesha upatikanaji wa vipimo sahihi vya maji ambapo imeweza kuhakiki dira700, 000 za maji.

 

“Katika kuboresha sekta ya maji Serikali iliipatia WMA kiasi cha shilingi milioni 500 ambazo zimesaidia kununua kifaa cha kisasa (water meter test bench) cha kuhakiki
dira za maji kabla hazijafungwa kwa wateja na mpaka sasa WMA imeweza kuhakiki dira za maji 700,000 ambapo kati ya hizo zilizopitishwa ni 570,000 na zilizokataliwa kutokana na kuwa na matatizo ni 130,000”, Dkt.Manege.

 

Aidha Dkt. Manege alisema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli, WMA imeweza kutoa gawio la TZS bilioni 12.5 mara baada ya
kuwezeshwa na kununua vifaa vya kisasa vinavyotoa huduma bora kwa wafanyabiashara na wateja wao.

 

Mpaka sasa WMA imepiga hatua kubwa ya kuwa na wazalishaji wa ndani zaidi ya 15 (viwanda vidogo) wanaotengeneza mizani zenye usahihi mzuri na kulete usawa katika biashara, pia WMA imeweza kununua magari 30 ambayo yamesambazwa katika mikoa yote nchini kwa ajili ya kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.