………………………..
Na. John Bera – Mvomero
WIZARA ya Malisili na Utalii kupitia Idara ya Misitu na Nyuki imeendelea na juhudi za kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhifadhi misitu, ufugaji nyuki, na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla. Katika kuendeleza juhudi hizo, Idara imetembelea programu ya Eco-School ambayo inatekelezwa na Shirika la kuhifadhi misitu ya asili Tanzania (TFCG). Programu hiyo inatekelezwa katika Kijiji cha Kwelikwaju, Turiani, Wilaya ya Mvomero. Programu hii imekuwa ikitoa elimu kwa vitendo kwa wanafunzi kuhusu uongozi, kilimo, utunzaji wa misitu na mazingira kwa ujumla.
Haya yameelezwa na Afisa Misitu Mkuu kutoka Idara ya Misitu na Nyuki ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Emmanuel Msoffe mara baada ya kutembelea Shule ya Msingi Kwelikwiji iliyopo Tarafa ya Turiani wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro ambayo inatekeleza mradi wa ufugaji nyuki chini ya programu ya Eco-School.
Amesema rasilimali za misitu na nyuki zina mchango mkubwa kiuchumi, kijamii na kimazingira na hivyo kwa shule hii imefanikiwa kupitia wanafunzi kuweza kupata nishati, hewa safi, kulinda vyanzo vya maji na upatikanaji wa majengo. Pia, Program hii imesaidia upatikanaji wa asali ambayo ni chakula na huduma ya uchavushaji.
Msoffe amesema sekta ya misitu inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upanuaji wa maeneo kwa ajili ya kilimo, uchomaji wa moto, uvunaji haramu wa mazao ya misitu ambayo huchangia upotevu wa misitu kwa kasi kubwa ambapo hupoteza Tanzania takribani hekta 496,000 kwa mwaka.
Amesema katika kukabiliana na hali hiyo, Wizara imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kudhibiti upotevu wa misitu ikiwemo ya utoaji elimu ya umuhimu wa utunzaji wa misitu kwa wananchi hususani vijana wadogo.
“Ili kupata watunzaji wazuri wa misitu ni vizuri kuanzia kwenye ngazi ya chini kabisa kwenye elimu ya msingi ili wakiwa wazazi washiriki kwenye utunzaji wa misitu kikamilifu”
Msoffe amesema katika kutekeleza hilo, Wizara inatekeleza Programu ya Eco-School ambayo imelenga kuwajengea uwezo watoto namna ya kutunza mazingira, misitu na ufugaji nyuki.
“Hatua hii inasaidia sana kuwa na watunzaji wazuri wa mazingira na hivyo kuchangia kwenye usimamizi endelevu wa misitu kwa kizazi cha sasa na kizazi kijacho.”
Naye Mkuu wa Shule ya Msingi Kwelikwiji, Evans John Mwerondo amesema shule yake inatekeleza miradi 11 ikiwamo ya kilimo cha kokoa, vanila na pilipili manga na ufugaji wa nyuki.
Amesema kupitia programu ya Eco-School wamefuga nyuki na kuna mizinga 12 na tayari shule imeanza kupata manufaa ya ufugaji nyuki huo ikiwamo kutunza uoto wa asili.
Amesema pia wamezalisha asali ambayo imesaidia kuiingiza shule kipato kinachotumika kununua chakula kwa ajili ya wanafunzi.
“Tunaishukuru Serikali, wizara na wadau kwa kutuwezesha kutekeleza programu ya Eco-School kwani kupitia programu hii shule inapata mapato na kufundisha wanafunzi somo la stadi za maisha.”
Naye mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Kwelikwiji, Goodluck John Exaver amesema kupitia ufugaji wa nyuki wameweza kuzalisha asali na mishumaa na kuwa ujuzi alioupata ameuhamishia nyumbani ambapo sasa nako wanafuga nyuki..