Kamishna wa Elimu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Lyabwene Mtahabwa amewataka wazazi na Wadau kote nchini kuwalinda watoto kwani ndio Tanzania ya kesho.
Mtahabwa ameyasema hayo wakati akifungua Kongamano la Kitaifa la Utoaji wa Chakula na Lishe Shuleni katika hoteli ya Morena Jijini Dodoma leo tarehe 25 Julai, 2024 kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda.
“nasema hivi zipo rasilimali nyingi Mungu ametupa, lakini nasema hivi, linda sana rasilimali watoto kuliko rasilimali zote unazolinda kwa maana hao ndio watakoamua Tanzania yetu ya kesho iweje, usikubali mtoto wako achezewe kwa namna yoyote ile” alisema Dkt. Mtahabwa.
Mtahabwa amesema lengo la kongamano hilo ni kukaa pamoja kama wataalam na kujadili kuhusu suala la lishe na chakula shuleni ili kuimarisha ujifunzaji wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari hapa nchini lakini kuhakikisha hakuna Mdau anayeachwa nyuma.
Akitoa salamu kabla ya hotuba ya mgeni rasmi Bw. Ernest Hinju Kaimu Mkurugenzi Idara ya Usimamizi wa Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI ameahidi kuyafanyia kazi maoni ya Wadau pamoja na kushirikiana nao Pamoja na kuimarisha jukumu la kusimamia na kushauri suala la chakula kwa shule za bweni na kutwa ili kuimarisha ujifunzaji.
Naye Vick Macha Naibu Mkurugenzi Mradi wa Tuwasilishe Pamoja amesema mradi huo wa miaka 5 unatekelezwa kwenye shule 367 kwa mkoa wa Mara na Dodoma ukiwa na lengo la kuwafikia wanafunzi 316,000 hali wakifanya kazi kwa kuhusisha jamii kuhusu miundo iliyopo ya ununuzi na uhifadhi chakula pamoja na kuhamasisha jamii kuchangia ili kuimarisha upatikanaji wa chakula na lishe shuleni.
Kwa upande wake Debora Esso Mwakilishi kutoka Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Tanzania amesema shirika lake linatoa ushauri wa kiufundi juu ya utoaji wa chakula na lishe shuleni na wanaendelea kuijengea uwezo Tanzania kuhusu masuala ya lishe shuleni wakishirikiana na shirika la chakula Duniani (FAO) na Serikali.
Kongamano la Kitaifa la Utoaji wa Chakula na Lishe Shuleni linafanyika kwa mara ya kwanza kwa siku mbili lenye kauli mbiu “Huduma ya chakula na lishe shuleni kwa afya na elimu bora” likiwahusisha Wadau kutoka Wizara za Kisekta, Taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali, mashirika ya Kitaifa na Kimataifa, makampuni binafsi, wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na Wadau wengine wa elimu wanaohusika na masuala ya lishe shuleni.