…………………
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano Mkuu wa pili wa Wahasibu wakuu wa serikali wa bara la Afrika(AAAG) unaotarajiwa kufanyika desemba 2 hadi 5 katika ukumbi wa mikutano wa Aicc mkoani Arusha .
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha kuhusiana na mkutano huo,Mhasibu Mkuu wa serikali CPA .Leonard Mkude amesema kuwa,mkutano huo unafanyika kwa mara ya pili tangu kuanzishwa kwake julai 5,2023 ambapo kwa mara ya kwanza ulifanyika nchini Lesotho febuari 2024.
Amesema kuwa , Umoja wa Wahasibu Wakuu wa serikali Afrika ulizinduliwa rasmi Mombasa,Kenya julai 5 ,2023 baada ya Azimio la kufunga Umoja wa Wahasibu uliokuwepo katika kanda mbalimbali, ambapo kwa sasa nchi 55 za umoja wa Afrika ni mwanachama wa Umoja huu.
“Lengo la Mkutano wa kimataifa wa Wahasibu ni kujenga imani ya Umma katika mifumo ya usimamizi wa fedha za Umma kwa ukuaji endelevu.”amesema .
Aidha ameongeza kuwa , inakadiriwa kuwa watu zaidi ya 2000 watashiriki mkutano huo wakiwemo Wahasibu,Wakaguzi wa hesabu, Wataalamu wa masuala ya fedha, Tehama,Vihatarishi n.k ambapo walengwa hao ni wale walioajiriwa serikalini, makampuni binafsi pamoja na waliojiajiri.
Ameongeza kuwa ,mkutano huo utawaleta pamoja wahasibu wakuu wa serikali wa Afrika watakaofuatana na Wahasibu wakuu wa wizara,Taasisi za umma ,wahasibu wa ngazi tofauti tofauti na wadau wengine ,kutoka nje ambao watakuja na fedha za kigeni ambazo watazitumia hapa Tanzania .
Amefafanua kuwa, wahasibu na wakaguzi wa hesabu watakaohudhuria watapata fursa ya kusikiliza mada za masuala mbalimbali ya kitaaluma ,sambamba na kukutana na wahasibu wakuu wa serikali wa Afrika na kubadilishana mawazo na kupeana mawasiliano,kujua fursa zinazopatikana katika nchi za kiafrika.
Aidha ametoa wito kwa wahasibu ,wakaguzi wa hesabu na wadau wengine wote hususani watanzania kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kuhudhuria mkutano huo mkubwa kwa njia ambazo zitatajwa huku kuwataka maafisa masuuli wa wizara na taasisi zote kuwaruhusu wahasibu na wakaguzi watakaoomba kuhudhuria mkutano huo.
Mwenyekiti wa Umoja wa wahasibu wakuu wa Afrika, Malehlohonolo Mahase,amesema kuwa,faida za mkutano huo ni pamoja na kuwa na Afrika yenye mafanikio yenye msingi wa ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu,bara jumuishi lililounganishwa kisiasa kwa kuzingatia maadili ya Pan-Africanism na maono ya mwamko wa Afrika,pamoja na kuwa na Afrika yenye utawala bora, demokrasia, kuheshimu haki za binadamu ,haki na utawala wa sheria .
Amefafanua kuwa baada ya mkutano huo wanatarajia kuwa na Afrika yenye amani na usalama na yenye utambulisho thabiti wa kitamaduni, urithi wa pamoja na maadili.
“Nchi ya Tanzania ina maswala mazuri ya uzalendo na kupitia mkutano huu tutaweza kujifunza maswala mazuri yanayofanywa na nchi ya Tanzania ikiwemo usimamizi mzuri wa fedha pamoja na kuja kuangalia fursa mbalimbali za uwekezaji.”amesema .
Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha AICC ,Christine Mwakatobe amesema kuwa ,wamejipanga vyema kuhakikisha wageni wanapokuja waweze kutoa huduma bora .
Aidha amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutangaza nchi yetu duniani kwani hiyo ni kazi kubwa aliyoifanya ya kutangaza utalii kwani wameona mikutano mingi na wawekezaji wanaendelea kuja .