WANANCHI wa kijiji cha Mbizi kata ya Mega, halmashauri ya Msalala wilayani Kahama Mkoani Shinyanga wamemuomba mbunge wa Jimbo la Msalala Iddi Kassim Iddi kusaidia kumaliza mgogoro wa eneo lenye hekari 231 linalodaiwa kutolewa kwa matumizi ya kijiji na mzee Petro Ngaluka.
Ombi la wananchi hao linakuja kufuatia Mzee Petro Ngaluka kudai kipande cha eneo ambalo limechukuliwa na serikali ya kijiji hakulitoa na kwamba wamevuka mipaka tofauti na makubaliano ya hapo awali.
Taarifa ya serikali ya kijiji inaeleza takribani hekari 231 zilitolewa na familia sita ambazo zipo kijijini hapo ikiwemo ya mlalamikaji Petro Ngaluka, huku wengine ni Ng’ombe Mabula, Sengerema Malale, Samadali Magina na Mapula Lugahila.
“Mheshimiwa Mbunge tunakushukuru kwa kuweza kufika na kusikiliza kero zetu lakini hapa kijijini kwetu kuna shida ya mgogoro wa eneo la kijiji ambalo lilitolewa kwa hiyari na Petro lakini amegeuka na kutaka eneo lake lirudishwe sasa tumekuwa na wasi wasi mkubwa hapa kijijini mtu ametoa kwa hiyari yake kwa ajili ya maendeleo.
“Cha kushangaza wenzake hawajawahi kudai kukatiwa vipande leo yeye anataka akatiwe kipande kirudishwe kwake tunakuomba suala hili Mbunge utusaidie.” Alisema Joseph Kayagamba.
Kufuatia madai hayo mtoto wa mdai wa eneo ambaye anafahamika kwa jina la Mathias Ngalula amesema eneo ambalo alitoa mzee wake miguu (hatua) 70 upana na urefu ukiwa ni hatua 800 lakini viongozi wamekuwa wakitaka kumnyang’anya na eneo ambalo ni mali yake tofauti na makubaliano.
Baada ya kusikilia madai hayo, Mbunge wa Msalala Iddi Kassim Iddi, amewaomba uongozi na wakazi wa kijiji hicho kuona uwezekano wa kufikiria maombi ya mzee Ngalula na kama haitawezekana basi uongozi wa kijiji umruhusu mzee kupeleka madai yake kwenye baraza la ardhi.
“Niwaombe kijiji waiteni wale waliotoa maeneo waje waandike upya tena na sio muhtasari tu ikiwezekana tusajiri kwenye baraza la kijiji na ikiwezekana tukachukue hati ya kijiji itasaidia kujua umiliki halali upo kwenye upande wa nani.” Alisema Iddi Kassim.