NA EMMANUEL MBATILO
Serikali imesema kutokana kuwapo kwa uhaba wa samaki nchini imeweka mikakati ya kuongeza kasi ya ufugaji wa samaki hao kwa ajili ya kutosheleza katika soko la ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Ukuaji wa viumbe hai wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Midala amesema kuwa wastani mtu mmoja anatakiwa kula samaki Kilogramu 20 kwa mwaka, lakini nchini mtu mmoja anakula Kilogramu 7.9 kwa mwaka wakati samaki ana virutubisho vingi katika mwili wa binadamu.
“Nchini tani 350,000 hadi 380,000 za samaki zinazalishwa kwa mwaka ambazo hazitoshelezi kulingana na mahitaji yaliyopo na kukabiliana na na uhaba wizara inahimiza wavuvi na wadau wengine kujikita kwenye ufugaji wa samaki,” amesema Dk. Madala.
Aidha Dkt. Madala amesema kupungua kwa samaki kunatokana na kuwepo kwa uvuvi haramu, uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi na kufanya samaki kupungua kwa zaidi ya miaka 20 bila kuongezeka.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama Cha Wakuzaji wa Viumbe Maji Tanzania(AAT),Geoffrey Rucho, amesema lengo la mkutano huo ni kuhakikisha utafiti uliofanywa kuhusu hali halisi ya viumbe hai nchini na kuwakutanisha wadau kujadili kutaleta mabadiliko chanya katika sekta hiyo kwa kuongeza uzalishaji wa samaki na kufikia malengo ya wizara.
Hata hivyo kwa upande wa Mtaalamu wa viumbe hai, Profesa Philip Bwathondi, alisema viumbe hao wa majini kama samaki wamepungua kwa sababu watumiaji wameongezeka na vifaa vya kuvulia vimeongezeka.
Amesema njia ya kuongeza viumbe hao ni kuanza kufuga na kusaidia wavuvi wengine kujikita kwenye kufuga na kuongeza uzalishaji.
Bwathondi Amesema njia nyingine ni kufuga samaki wadogo ambao wakifika umri wa ukuaji wanamwagwa kwenye eneo moja la ukuaji ili kupunguza upungufu uliopo, kwani kuna tofauti ya samaki wa baharini na wakufungwa, wale wanaofugwa ni wazuri zaidi kwa sababu wanapewa vyakula bora.