Serikali ya Tanzania ipo katika hatua ya kupitia upya sheria ya fidia ya uharibifu unaofanywa na wanyamapori ili kuendana na wakati na gharama halisi ya mazao yanayoharibiwa na wanyama hao ili kupunguza malalamiko ya wananchi juu ya kutokupewa fidia stahiki inayoendana na uharibifu hao.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ,Profesa Adolf Mkenda wakati akizungumza katika mkutano wa wadau wa uhifadhi na maliasili uliondaliwa na Jumuiko la Maliasili nchini Tanzania (TRN) ,ambapo amesema kuwa sheria hiyo ya mwaka 1974 inafanyiwa mapitio na kufanyiwa marekebisho ili wananchi waweze kupata haki pale uharibifu unapotokea.
Profesa Mkenda asema kuwa marekebisho yatakayofanyika yataweza kupunguza malalamiko yaliyokua yakitolewa na wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi lakini pia wizara hiyo imekua ikigawa mizinga ya nyuki kama njia mojawapo ya kukabiliana na uharibifu wa wanyamapori hususan tembo.
Aidha amesema kuwa katika kukabiliana na uwindaji wa kitoweo baada ya kufanikiwa kutokomeza uwindaji haramu wa tembo kwa sasa wizara inakamilisha mchakato wa kuwa na sehemu za kuuza nyama pori katika maeneo yanayozunguka hifadhi ili kuepuka uwindaji wa kitoweo katika maeneo ya uhifadhi.
Mbunge wa Babati Vijijini Jitu Soni amesema kuwa kurekebishwa kwa sheria ya fidia kutawafuta wananchi machozi hasa wanaoishi mbali kidogo na hifadhi tofauti na wale walioko karibu na pia itasaidia kuhamasisha uhifadhi endelevu miongoni mwa wananchi.
Mkurugenzi wa Jumuiko la Maliasili nchini Tanzania Zacharia Faustine amesema kuwa mchakato wa kulipa fidia umekua ukichukua muda mrefu na kiasi wanacholipwa hakiendani na hasara jambo ambalo linaweza kushusha hamasa wa wananchi kushiriki katika uhifadhi hivyo serikali imefanya vyema kupitia sheria hiyo.
Mmoja wa wananchi wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi za taifa,Asha Salim amesema kuwa marekebisho sheria ya fidia imekua sio rafiki kwa wananchi hivyo inapaswa kuangaliwa upya kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.