Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Kagera
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) amewataka wananchi wa vijijini waliofikishiwa huduma za mawasiliano kuipa thamani miradi hiyo kwa kuitumia vinginevyo uwekezaji uliofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Sekta binafsi hautakuwa na maana.
Waziri Nape ametoa kauli hiyo tarehe 16 Julai, 2024 mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa Mnara wa mawasiliano katika Kijiji cha Kisharara, Kata ya Karambi wilayani Muleba, mkoani Kagera akiwa katika siku ya pili ya ziara yake kwenye Mikoa ya Kanda ya Ziwa.
” Niwahakikishie tu utayari wa Serikali kuendelea kufanya kazi na sekta Binafsi, kwenye hili la Mawasiliano nadhani tumefanikiwa sana, …. sekta binafsi inaleta fedha zake inafanya biashara, lakini Serikali inaongeza fedha miradi itekelezwe ili hawa wananchi ambao katika hali ya kawaida wasingefikiwa waweze kupata mawasiliano,” amesema Waziri Nape na kusisitiza;
“Wito wangu kwa wananchi moja watumie hizi huduma, kwa sababu kadri idadi yao inavyoongezeka inatusaidia kuona namna ambavyo gharama zitapungua lakini pia tunaupa thamani mradi huu, fedha iliyolazwa hapa (zaidi ya milioni 300) kama watumiaji watakuwa hawaongezeki inakuwa hasara kwa watoa huduma na kwa Serikali”.
Waziri Nape ameipongeza Kampuni ya Vodacom kwa kujenga minara imara na yenye uwezo mkubwa na kuitaka kuongeza nguvu ya kukopesha wanavijiji simu ili kuongeza idadi ya watumiaji wa huduma hizo.
Awali akizungumza na Viongozi wa Mkoa, wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara na watoa huduma katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Waziri Nape amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi mkoani humo kusimamia ipasavyo kodi ya pango katika maeneo yote yaliyojengwa Minara kwenye ardhi ya kijiji ili iwe na matokeo chanya na wananchi wanufaike na ardhi yao.
Akitoa taarifa ya mnara huo wa Mkuu wa Vodacom Kanda ya Ziwa Ezekiel Nungwi, amesema tangu mnara huo uwashwe Juni 21 mwaka huu tayari vijana Saba wamejiari kutoa huduma za Uwakala wa Mpesa na wengine kuuza line wakati jumla ya wanufaika wa mawasiliano ni watu 20,000.
“Mheshimiwa Waziri mnara huu umeshatoa ajira kwa mawakala saba na mzunguko wake tangu tumewasha mnara ni shilingi milioni 25 hadi 50, vilevile tumetoa ajira za muda mfupi kwa wajenzi ambao ni watu wanaotoka hapa hapa kijijini na ajira ya muda mrefu kwa Mlinzi,”
Waziri Nape pia amekagua minara katika Kijiji cha Kasharara Kata ya Karambi Wilaya ya Muleba na kijiji cha Katahoka Kata ya Katahoka Wilaya ya Biharamulo alikowasisitiza pia wananchi kutumia vizuri mitandao ili isivunje ndoa zao bali kuziimarisha.