Baadhi ya wajumbe wa kamati maalum ya kukagua mipaka ya kimataifa wakipokea taarifa ya kuhusu halisi ya mpaka wa Tanzania na Burundi.
…………..
Na: Eliafile Solla
Tanzania ni nchi ambayo iko vizuri na majirani zake kwa maana ya nchi zinazoizunguka na wananchi wake wanashirikiana vyema na majirani zao katika masuala mbalimbali ya kijamii na kimaendeleo kama vile biashara hasa ya kuuziana mazao. Haya yalithibitishwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ngara mkoani Kagera Vedastus Tibaijuka wakati alipokuwa anatoa historia ya mpaka wa Tanzania na nchi jirani ya Burundi kwa kamati maalum iliyojumuisha ofisi saba za Serikali walipofika Wilayani humo kwa lengo la kutembelea na kukagua mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Burundi.
Katika kuimarisha mipaka ya kimataifa kati ya Tanzania na nchi jirani zinazo izunguka, Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeunda kamati maalum kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wote wanaoishi kwenye vijiji vya mipakani wanakuwa salama pamoja na mali zao. Kamati hiyo maalum inahusisha Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ofisi ya Rais, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Nae mkuu wa Wilaya ya Ngara Lt. Kan. Michael Mtenjele aliieleza kamati hiyo maalum kwamba, Wilaya ya Ngara imegawanyika katika tarafa 4 zenye jumla ya kata 22, vijiji 75 na vitongoji 389. Alisisitiza kwamba, Wilaya ya Ngara iko mpakani kabisa mwa Tanzania na Burundi na hivyo siyo ajabu Watanzania kuwa na ndugu, jamaa na marafiki upande wa Burundi au Waburundi kuwa na jamaa Tanzania. Kwa sababu hiyo, wananchi hasa wa vijiji vya mpakani wanaishi vizuri na majirani zao na kushirikiana katika masuala mbalimbali.
Katika taarifa yake kuhusu hali halisi ya mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Burundi alisema, mpaka huo uko salama na changamoto zinapojitokeza hukutana katika vikao vya ujirani mwema na kuzitatua japo kuna baadhi ya wananchi kutoka Burundi huingia na kuishi upande wa Tanzania bila kufuata sheria na taratibu za uhamiaji.
Mkuu huyo wa Wilaya aliieleza kamati maalum kwamba, kwenye uimarishaji wa mpaka huo uliofanyika mwaka 2014, baadhi ya wanachi wa vijiji vya mpakani walijikuta wakipoteza baadhi ya mali zao kama vile nyumba na mashamba baada ya maeneo hayo kuonekana yako upande wa Burundi na siyo Tanzania. Hiyo imekuwa ni changamoto kwa sababu wananchi hao tayari walishakuwa na familia zao katika maeneo hayo na wengine hadi makaburi ya jamaa zao yapo upande wa Burundi na wao wanaishi upande wa Tanzania.
Nae kiongozi wa msafara wa kamati hiyo maalum Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ndugu Ramadhan Kailima, aliipokea taarifa hiyo kuhusu hali halisi ya mpaka wa Tanzania na Burundi na kuahidi kwamba kwa pamoja kama kamati maalum watakaa na kuona ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia wananchi walioathirika na uimarishaji mpaka uliofanyika mwaka 2014 kwa maana ya wale ambao baadhi ya maeneo yao yalibaki upande wa nchi jirani ya Burundi.