Na Sophia Kingimali.
WAZABUNI wanaoomba zabuni za umma na wanapopata changamoto au kutoridhika na mchakato wa ununuzi wa umma wametakiwa kuwasilisha malalamiko yao katika chombo cha Mamlaka ya Rufani za Zabuni za Umma (PPAA),ili kupata haki zao.
Akizungumza katika banda la PPAA kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando amesema chombo hicho kipo kwa ajili ya kusikiliza na na kutoa suluhu ya malalamiko ya wazabuni itokanayo na michakato ya ununuzi wa umma.
Amesema wamepokea malalamiko yote kuhusu zabuni za umma,wanachofanya ni kusikiliza na kuyatafutia ufumbuzi na mengi wameyamaliza na haki imetendeka.
Amesema katika maonesho hayo wametembelewa na watu wengi waliopewa elimu na wengine kuelimishwa utaratibu wa kuwasilisha malalamiko yao na kusema bado elimu inahitajika kwa wananchi wengi kufahamu mifumo ya kufuata endapo wana malalamiko.
Vilevile amesema kwa sasa wazabuni wote wanaoomba zabuni za ununuzi wa umma ni lazima watumie mfumo mpya wa kielektroniki wa manunuzi ya Umma ( NeST) kama sheria inavyotaka baada ya kuwasilisha maombi yake hufanyiwa kazi na kupata majibu.
Sando amesema mfumo huo ni rafiki na rahisi kwa sababu umerahisisha utoaji huduma kwa wazabuni badala ya kuwasilisha zabuni zao ana kwa ana sasa wanawasilisha kwa mtandao na hiyo inapunguza gharama na kuokoa muda.
Pia amesema kwa sasa PPAA inakamilisha kanuni mpya za rufani za mwaka 2024.