Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Dkt. Hussein Mohammed Omar atembelea banda la Chuo Kikuu Mzumbe katika Maonesho ya Sabasaba ya mwaka 2024 yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu J. K. Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam. Pamoja na kutembelea banda hilo, Dkt. Hussein amepongeza bunifu mbalimbali zinazooneshwa na Chuo hicho katika Maonesho hayo ya Kimataifa ya Sabasaba. Amesema Wizara ya Kilimo iko tayari kuwainua vijana hususan wabunifu katika sekta ya Kilimo.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya Bw. Gerald Cosmas Mabuto akielezea kuhusu ubunifu wake wa Kupanda migomba kwa kutumia ndizi mbivu asilia kama mbegu kwa baadhi ya watu waliotembelea banda la Chuo Kikuu Mzumbe .
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki Kuu Morogoro Bw. Yona Peter akielezea kuhusu ubunifu wake wa mfumo wa kuagiza vitu mtandaoni kwa njia rahisi kwa baadhi ya watu waliotembelea banda la Chuo Kikuu Mzumbe .
Mwakilishi wa Kitivo cha Sayansi na Teknolojia Chuo Kikuu Mzumbe Bw. Frank Msonge akielezea kuhusu ubunifu wa mfumo wa kujaza maji kwenye tenki kwa njia ya sms kwa baadhi ya watu waliotembelea banda la Chuo Kikuu Mzumbe.
……….
Chuo kikuu Mzumbe ni moja kati ya vyuo vikubwa na kongwe nchini Tanzania ambacho kimepata nafasi ya kushiriki maonesho ya 48 ya biashara ya kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Mwl. J. K. Nyerere maarufu kama sabasaba.
Katika maonesho hayo moja ya vitu vilivyoonekana kuvutia wageni wanaotembelea banda hilo ni pamoja na bunifu mbalimbali zilizofanywa na wanafunzi wachuo hicho baada ya kuonyesha vipaji vyao na kulelewa kwa usimamizi mkubwa na wakaribu kutoka kwa walimu wao.
Kupanda migomba kwa kutumia ndizi mbivu kama mbegu ni ubunifu wa Bw. Gerald Cosmas Mabuto kutoka chuo kikuu Mzumbe ndaki ya Mbeya imekuwa ni kivutio cha wageni wengi wenye kupenda kilimo na hata wale ambao sio wakulima.
Njia hii ya kupata miche mingi zaidi ya migomba ndani ya muda mfupi na yenye uwezo wa kuzaa matunda zaidi haijavutia wageni tu bali hata taasisi mbalimbali za umma na zile za binafsi zinazojishughulisha na kilimo pamoja tafiti ikiwemo TARI na Wizara ya Kilimo.
Ubunifu mwigine ni wa Bw. Yona Peter mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu Mzumbe ndaki ya Morogoro ambae amebuni mfumo wa kuagiza vitu mtandaoni kwa njia rahisi umeonekana kuwavutia vijana wengi zaidi hasa wanaojihusisha na biashara na wale walioko masomoni.
Mfumo huu ambao pia umeonekana unaoweza kutumika kwa wafanyakazi wa maofisini kuagiza chakula na kuletewa bila wao kuacha shughuli zao umeonekana kuokoa muda mwingi unaopotea wakati wa mapumziko ya chakula lakini pia unampa mtumiaji uhuru na wigo mpana zaidi wa kuchagua anachotaka kwa wepesi.
“Hakika maji ni rasilimali muhimu inayotakiwa kutunzwa sana, napongeza sana ubunifu huu wa kuzuia upotevu wa maji hasa majumbani” alisema Bw. Makame Hussein baada ya kupata maelekezo juu ya mfumo wa kujaza maji kwenye tenki kwa kutumia sms kwa njia ya simu.
Ubunifu huo kutoka Kitivo cha Sayansi na Teknolojia Chuo Kikuu Mzumbe kampasi kuu Morogoro umebuniwa na Bw. Frank Msonge ambaye amesema kuwa ubunifu huo bandani hapo umekuwa kivutio kwa wageni wengi waliotembelea banda la Chuo kikuu Mzumbe katika maonesho ya 48 ya saba saba.
Mfumo huu wenye kusaidia ujazaji wa maji kwenye matenki na kufunga yanapojaa kwa kutumia simu hata mtumiaji anapokuwa mbali na eneo la nyumbani au ofisi, umeonekana bora zaidi katika kuhakikisha upotevu wa maji pia kupunguza usumbufu mkubwa kwa mtumiaji.
Hakika bunifu za chuo kikuu Mzumbe zimeonekana kuendana na kasi ya ukuaji wa sayansi na tekinolojia katika karne hii ya 21.