Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Mbeya, Edina Mwaigomole akizungumza na wajumbe wa Baraza la Jumuiya la Mbeya mjini wakiwa kwenye kikao cha Balaza la kawaida kilichofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Mbeya Day jijini humo.(Picha na Joachim Nyambo)
………………..
Na Joachim Nyambo, Mbeya.
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) mkoani Mbeya wametakiwa kutambua kuwa kulipa ada ni miongoni mwa mambo muhimu na yenye kudumisha uhai wa chama.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Mbeya, Edina Mwaigomole alisisitiza hilo alipozungumza na wajumbe wa Baraza la Jumuiya la Mbeya mjini kwenye kikao cha Balaza la kawaida kilichofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Mbeya Day jijini hupa
Mwaigomole alisema bado wapo wanachama wanaoamini kujiunga na uanachama inatosha na hivyo kutozingatia ulipaji wa ada ya kila mwaka dhana aliyosema inapaswa kundoka kwenye mawazo ya kila mwanaCCM.
“Tunapozungumza uhai wa chama ni lazima wewe mwenyewe uwe uko safi.Tuhamasishane chama ni ada … mbona hata vikoba vyetu tunachangia na ndiyo vinakuwa imara.. tusipochangia si tunaona vinakufa?”
“Wengine hawaelewi wanafikiri ukiwa mwanachama basi…sasa unafikiri chama kitaendeshwa na nini? Kila mmoja ajitahidi kutoa elimu kwa hawa walio chini yetu.”
Mwenyekiti huyo pia aliwasihi wajumbe na viongozi kuwasaidia wanawake wanachama wa CCM kuinuka kiuchumi kwa kuwajengea uwezo na pia ubunifu wa shughuli mbalimbali za ujasiriamali ili kuimarisha vipato vyao.
Kwa upande wake Mbunge wa viti maalumu Suma Fyandomo aliwataka wanawake kuhamasika kuwania nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ili kuongeza idadi ya kundi hilo kwenye vyombo vya maamuzi.
Hata hivyo alisisitiza umuhimu wa wagombea kuwa walio na vigezo stahiki ili watakapochaguliwa wawe na sifa zinazokidhi vigezo vya kuwa viongozi watakaowatumikia wananchi kwa weledi.
“Kwanza tuhamasishe tukiona mtu anasifa anatosha achukue fomu. Asiwepo mtu yeyote wa kumrudisha nyuma ”