Na Sophia Kingimali.
Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Taifa la bima NIC Kaimu Abdi amesema kufuatia uwekezaji unaondelea nchini wawekezaji wanapaswa kukata bima za biashara zao ili pindi majanga yanapojitokeza waweze kufidiwa.
Akizungumza leo Julai 9,2024 jijini Dar es salaam mara baada ya kutembelea kwenye banda la NIC lilipo kwenye maonesho ya 48 ya biashara ya kimataifa amesema shirika limekuwa likitoa bima mbili muhimu kwa ustawi wa nchi.
Akizitaja bima hizo amesema ni bima za maisha na bima sizizo za maisha ambapo bima zisizo za maisha zinaenda moja kwa moja na kauli mbiu ya maonesho hayo isemayo Tanzania mahali salama pa biashara na uwekezaji’
“NIC hili ni shirika la umma hivyo tunatoa bima aina mbili za maisha na zisizo za maisha ambazo hizi zinawagusa moja kwa moja wawekezaji kwani mwekezaji akipata majanga tunaweza kuwafidia na wakaendelea na uwekezaji wake kama kawaida”,Amesema.
Amesema pamoja na kuwa ni Taasisi ya serikali lakini pia wanafanyabishara kwani wanajukumu la kulipa kodi lakini wanajukumu kubwa la kuwahudumia Watanzania.
Akizungumzia mikakati waliojiwekea katika mwaka huu wa fedha kuhusu kutoa uelewa kwa wananchi amesema wamejipanga kuwafuata wananchi walipo na kuwapa elimu ya Bima.
“Tulichogundua wananchi wengi hawana elimu ya bima sasa tumejipanga kuhakikisha tunawafuata huko huko walipo na kuwapa elimu hii maana bima ni muhimu na uwezi kuona umuhimu wake kama hayajakukuta sasa hatusubiri yakukute tutahikikisha elimu inamfikia kila mmoja ili waweze kujiunga na Bima”,Amesema.