NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeanza kutekeleza Kampeni ya ‘Zinduka, Usiumizwe, Kopa kwa Maendeleo’ ambayo imelenga kutoa elimu kwa jamii kuhusu kuzingatia utaratibu kabla ya kukopa fedha katika taasisi yoyote jambo ambalo litasaidia kupunguza migogoro isiyokuwa ya lazima.
Akizungumza na mwandishi wetu katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam, Afisa Mkuu
Mwandamizi, Kurugenzi ya Usimamizi Sekta ya Fedha, Idara ya huduma ndogo ya Fedha, Bw. Deogratius Mnyamani, amesema kuwa changamoto iliyopo kwa sasa ni uelewa mdogo kwa watoa huduma wa mikopo ya fedha pamoja na watumiaji.
Bw. Mnyamani amesema kuwa kulitambua hilo BoT imekuja na kampeni ‘Zinduka, Usiumizwe, Kopa kwa Maendeleo’ ili kuhakikisha elimu inafika kwa watanzania.
“Tumekuja na kampeni hii tumeona wakopaji wengi wanachukua mikopo bila kuzingatia vitu vya muhimu, kampeni inatoa elimu kwa mkopaji ili kuwa na uelewa mkubwa kabla ya kuchukua mkopo” Bw. Mnyamani.
Amesema kuwa vitu vya muhimu ambavyo mkopaji anapaswa kuzingatia ni kukopa katika taasisi zenye leseni pamoja na kujua vigezo na masharti ya mkopo huo.
“Tumegundua watu wengi wanaopata shida baada ya kukopa kwa sababu hawakupata muda kueleweshwa kuhusu vigezo na masharti wakati wanachukua mikopo, kampeni hii inakwenda tunatoa elimu ili mkopaji apate muda wa kusoma mkataba pamoja na kupata ushauri kabla ya kuchukua mkopo” amesema Bw. Mnyamani.
Amesema kuwa watoaji wa mikopo wengi hawafauati taratibu ikiwemo kutoa nakala ya mkataba iliyosainiwa licha ya kuwa ni haki ya mkopaji .
Bw. Mnyamani amesema kuwa nakala ya mkataba ni muhimu kwa mkopaji kwani unaweza kumsaidia pale inapotokea changamoto ya kutaka kuzulumiwa mali zake na mtoa huduma.
Aidha amefafanua kuwa BoT kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Jeshi la Polisi wanaendelea kuwatafuta watoa huduma ya mikopo ya fedha kwa njia ya mtandao ambao wamevunja sheria ya uhuru wa mtu binafsi pamoja na kumtangaza vibaya mkopaji.
“Tumetoa maelekezo mtu yoyote anayefanya biashara ya kutoa mikopo mtandaoni licha ya kuwa na leseni anapaswa kufika BoT kupewa idhini nyengine ya kufanya biashara mtandaoni, tunatatoa idhini baada ya kujiridhisha mwenendo wa mtoa huduma” amesema Bw. Mnyamani.