Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
WATEJA waliokuwa wameweka fedha kwenye Benki ambazo zimefilisiwa na Benki Kuu ya Tanzania BoT wametakiwa kwenda kuchukua stahiki zao za Fidia ya Amana ya Sh.Milioni 1.5 bodi ya bima ya Amana DIB.
Hayo yameelezwa na Afisa Benki kutoka Bodi ya Bima ya Amana DIB Twaiba Juma wakati akizungumza na Fullshangweblog katika maonesho ya Biashara ya kimataifa yanayoendelea kwenye viwanja vya Sabasaba Barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam ambapo amesema lengo la Taasisi hiyo ya Serikali ni kumlinda mteja pale ambapo benki au taasisi inayoweka fedha zake inaweza kufungwa kutokana na majanga tofauti au kufutiwa leaeni pamoja na kufilisika.
Amesema kwamba kazi za Bodi ya Bima ya Amana DIB ni kusimamia mfuko wa Bima ya Amana ambayo wachangiaji wakubwa ni mabenki na Taasisi za fedha zenye leseni kutoka BoT ambapo michango tunayoipokea tunaikuza kwa kuwekeza kwenye dhamana ya serikali na hii inasaidia mfuko kukua.
“Ndio maana baada ya muda tumeongeza kiwango cha fidia kutoka shilingi Milioni 1.5 mpaka shilingi Milioni 7.5 kiwango ambacho kitakuja baada ya benki kuanguka sasa hivi kiwango hicho bado hakijatumika kutokana na kwamba benki bado ziko imara“Amesema .
Twaiba amesema lengo la Taasisi hiyo ni kuchangia katika kujenga uimara uadilifu na imani kwa jamii katika mfumo wa fedha nchini kwa kutoa bima au kinga kwa amana stahiki kwa wateja wa benki husika.
Amesema kwamba bima hiyo inatolewa wakati Benki Kuu ya Tanzania inaifutia leseni benki au taasisi ya fedha na kuichagua bodi ya bima ya amana kama mfilisi wa benki au taasisi hiyo na wao kama mfilisi wanakuwa na jukumu la kulipa fidia kwa wateja pale ambapo benki au taasisi ya fedha imefilisika.
Amesema kwa sasa kiasi cha juu cha fidia ambazo wanatoa ni Milioni 7.5 ambacho kimeanza kutumika mwezi February mwaka 2023 na hiyo ni ongezeko kutoka kiwango cha awali cha milioni 1.5 na tokea waongeze kiwango hicho hakuna benki yoyote iliyofilisika na wameona benki zimeendelea kuwa imara katika sekta ya fedha na benki kuu akiendelea kufanya majukumu yake ya kusimamia sekta ya fedha kwa ufasaha zaidi.
Ameongeza kwamba mbali na kiwango kipya katika kiwango cha zamani cha milioni 1.5 kuna benki ambazo zipo kwenye ufilisi maana DIB imechaguliwa na BoT kuwa mfilisi ambapo katika ufilisi huo wapo wateja ambao hawajachukua hiyo fidia ya amana wapo wateja kwa upande wa Milioni 1.5.
Amewataka wateja wa benki ambazo zimefilisika ambao bado hawajajitokeza kwenda kuchukua fidia zao wajitokeze kuchukua stahiki yao ya fidia ya amana katika benki Kuu ya Tanzania BoT Dodoma na Dar es Salaam
Amezitaja benki zilizofilisiwa ambazo wateja wake wanatakiwa kwenda BoT kuchukua fidia zao kuwa ni EFATA, Njombe Community Bank , Convenat Bank , FMB Bank, Kagera Farm Cooperative Bank ,Mbinga Community Bank na Meru Community Bank.
Katika hatua nyengine amewataka waliokopa kwenye Benki ambazo zimefilika hapa nchini kwenda kwenye bodi hiyo ili wapate taratibu za kurudisha mikopo hiyo kwa maana hiyo ni haki ya wateja wanaodai stahiki zao.
Amesema kwa maana wapo watu ambao wanadhani kwamba benki zinapokuwa zimefilisika basi madeni wanayodaiwa hawapaswi kuyalipa hilo sio jambo la kweli ni lazima wayalipe ili fedha hiyo ilipwe kwa wale waliokwa na stahiki zao katika benki hizo.
“Labda niwaambie waliokopa kwenye benki ambazo zimefilisika mnatakiwa muende mje kwenye bodi hii mpate taratibu za kurudisha mikopo yenu kwa maana hiyo ni haki kwa wateja ambao wanadai stahiki zao”Amesema