Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Deogratius Ndejembi amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutokana na kupata mafanikio mbalimbali katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya awamu ya sita.
Mhe. Ndejembi amesema hayo tarehe 7 Julai alipotembelea banda la NSSF katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu SabaSaba,ambapo amesema kuwa wakati Serikali ya awamu ya sita inaingia madarakani thamani ya NSSF ilikuwa trilioni 4.9 lakini sasa imekuwa hadi kufikia zaidi ya trilioni 8. Na hivyo kuthibitisha kazi kubwa inayofanywa na uongozi wa NSSF.
Pia Mhe. Ndejembi amesema kwamba amefurahi kuona kuwa tayari NSSF wana mikakati madhubuti ya kuwafikia wanachama waliojiajiri kupitia sekta isiyo rasmi, kwasababu kundi hilo lina umuhimu wa kuwa wanachama wachangiaji wa NSSF ili watakapokosa nguvu za kufanya kazi au kufanya uzalishaji mali wanufaike na mafao mbalimbali yanayotolewa na NSSF.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala wa NSSF, Bwana Ekwabi Mujungu amesema NSSF itaendelea kuwajengea uwezo watumishi wake ili kuhakikisha kuwa wanaendelea kutoa huduma bora kwa wanachama na wadau wote,na kuongeza kuwa NSSF inaungana na Serikali ya awamu ya sita katika mapambano dhidi rushwa hivyo ni vizuri wanachama kufuata utaratibu pindi wanapo hitaji huduma mbalimbali, huku baadhi ya wanachama waliotembelea banda la NSSF wakielezea kufurahishwa na huduma zilizoboreshwa kwa namna mifumo ya TEHAMA ilivyorahisha upatikanaji wa huduma hizo za NSSF.