Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) unatarajiwa kufanyika tarehe 11 na 12 Julai 2024 jijini Lusaka, Zambia.
Mkutano huo umetanguliwa na Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu unaofanyika tarehe 08
na 09 Julai 2024 jijini hapa ambapo ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huu unaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo.
Mkutano wa 26 unalenga pamoja na mambo mengine kujadili agenda mbalimbali zenye lengo la
kukuza na kuimarisha hali ya siasa, ulinzi na usalama katika Kanda ya SADC.
Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Makatibu Wakuu uliofanyika kwenye Ukumbi wa
Mikutano wa Kimataifa wa Mulungushi jijini Lusaka, Mwenyekiti ambaye pia ni Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Zambia, Bi. Etambuyu Gundersen
amewakaribisha wajumbe wa mkutano huo na kuwataka kujadili kikamilifu agenda mbalimbali zilizopo mbele yao kabla ya kuziwasilisha kwa Mawaziri.
Aidha, kuhusu hali ya usalama na amani katika Kanda ya SADC, Bi. Etambuyu amesema kuwa, hali ni shwari
huku akisisitiza kuendelea na jitihada za pamoja ili kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana katika maeneo machache yenye changamoto za kiusalama katika kanda ikiwemo eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kadhalika ametumia fursa hiyo kuzipongeza Jamhuri ya Afrika Kusini na Jamhuri ya Madagascar kwa
kuendesha kwa amani na utulivu zoezi la Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge lililofanyika katika nchi hizo hivi karibuni.
Mbali na Balozi Shelukindo, viongozi wengine kutoka Tanzania wanaoshiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe, Mkuu wa
Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Lt. Jen.
Mathew Mkingule, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Kamishna wa Polisi Salum Hamduni, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi.
Talha Waziri na Maafisa Waandamizi wa Wizara na Vyombo vya ulinzi na Usalama.