************************************
NA MWANDISHI WETU
TANZANIA ni nchi ya tatu kwa Afrika ikiongozwa na Nigeria kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa huo ambapo Tanzania inashika nafasi ya tatu na kila mwaka watoto takribani 11,000 uzaliwa na matatizo hayo.
Kutokana na ukubwa tatizo hilo, wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi(Muhas) wameamua kufanya utafiti na kutafuta njia ya kuutibu ikiwa ni pamoja na kupandikiza uboho(born marrow) na vinasaba kwenye mifupa.
SELIMUNDU NI UGONJWA GANI?
Kwa kawaida, chembe nyekundu ya damu ni mviringo, husafiri kupitia mishipa midogo kabisa ya damu kwa urahisi,na kwa wagonjwa wenye selimundu, chembe zao za damu huvunjika na kupoteza umbo hilo la mviringo na kuchukua umbo la ndizi au mundu(zana ya mkulima).
Chembe hizo nyekundu za damu zenye umbo la mundu hukwama katika mishipa midogo ya damu mwilini na mtiririko wa damu kwenda sehemu fulani ya mwili unapopungua huku oksijeni ikizuiwa na kusababiaha maumivu makali ya ghafla.
Kutokana na hali hiyo, maumivu makali katika mifupa na vifundo, maumivu yasiyotabirika ambayo yanaweza kutokea mara chache au mara nyingi kama kila mwezi kwa mgonjwa mwenye natatizo hayo.
Daktari wa watoto kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mloganzila, Mosses Karashani anasema kuwa hivi karibuni kumekua na ongezeko la rufaa kwa watoto wanaougua ugonjwa huo kuanzia miezi sita hadi miaka 14 ambapo kati yao, nusu ni wale walio chini ya miaka minane.
“Mtoto ambaye wazazi wao wote wawili(baba na mama) wana vinasaba vya selimundu, kuna uwezekano wa asilimia 25 kupata ugonjwa huo na mtoto ambaye mzazi mmoja hana vinasaba vya ugonjwa huo hawezi kupata ugonjwa huo,” anasema Dk. karashani.
Anaongeza kuwa, serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto walimua kuanzisha kliniki ya watoto wa ugonjwa huo siku ya Jumanne na Alhamisi hospitalini hapo ili waweze kupata huduma bora za matibabu.
Anasema kuwa, katika siku hiyo, zaidi ya watoto 20 wanafika hospitali hapo kupatiwa huduma za matibabu kuanzia umri wa miezi sita hadi miaka 14, ambapo kati yao, nusu yake ni wale wenye umri chini ya miaka 8, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa, tatizo la ugonjwa huo ni kubwa.
Anasema kuwa, watoto wanaougua kwenye ugonjwa huo baadhi yao wanapitia kwenye changamoto mbalimbali ikiwamo ya kukimbiwa na mzazi mmoja au unyanyapaa huku wazazi wengine wakizani mtoto wao amelogwa.
Anasema kuwa, katika nchi zinazoendelea ikiwamo Marekani na India, mtoto mara baada ya kuzaliwa anafanyiwa vipimo maalumu ‘screening’ ili kubaini matatizo aliyonayo, jambo ambalo linasaidia kuanza matibabu mapema kwa pale anapoonekana ana matatizo.
Anasema kuwa, vipimo hivyo ni muhimu kwa sababu vinasaidia kujua maradhi ambayo mtoto anaweza kuzaliwa nayo hivyo basi wakati umefika kwa Serikali kuboresha Sera za afya na kuanzisha mpango maalumu wa kuwafanyia vipimo maalumu watoto hao mara baada ya kuzaliwa.
Anasema kuwa, hali hiyo itasaidia kutambua matatizo ya mtoto kuanzia tumboni hadi anapozaliwa, jambo ambalo linaweza kupunguza ukubwa wa tatizo.