Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Kaspar Mmuya (kulia) akipokea kombe la msindi wa nne na cheti kutoka kwa Afisa Utumishi Mkuu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Lucy J. Timba (kushoto) ofisini kwake leo.
…….
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
VITENGO vya Mawasiliano Serikalini katika Mkoa wa Dodoma vimepongezwa kwa kuhabarisha wananchi juu ya kazi nzuri zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya Mkoa wa Dodoma kushika nafasi ya nne katika utoaji habari nchini kufuatia tathimini iliyofanywa na Idara ya Habari (Maelezo) chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari juu ya umahili wa utoaji habari kwa vitengo vya mawasiliano serikalini.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Kaspar Mmuya wakati akipokea zawadi ya kikombe na cheti baada ya Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kushika nafasi ya nne kati ya mikoa 26 ya Tanzania bara.
Mmuya alisema “napenda kuwapongeza kwa kazi nzuri ya kuhabarisha wananchi juu ya kazi na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Mkoa wa Dodoma. Hakika mmemuheshimisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Rosemary Senyamule. Nimefahamishwa kuwa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kimeshika nafasi ya nne, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Jiji la Dodoma kimeshika nafasi ya 13 na Halmashauri ya Mji wa Kondoa nafasi ya 15. Mwaka huu tulioanza tunataka kupiga hatua zaidi na kushika nafasi ya kwanza kwa sababu Dodoma ndiyo fahari ya watanzania”.
Alisema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipambanua katika kukuza uhuru wa habari ili wananchi waweze kupata habari sahihi. Habari sahihi zinapatikana katika vitengo vya mawasiliano serikalini. “Nimefurahishwa na umahiri wenu katika kuuhabarisha umma, matumizi ya mitandao ya kijamii na uhuishaji wa tovuti za serikali. Wito wangu kwenu endeleeni kujipanga zaidi ili habari na taarifa sahihi ziwafikie wananchi wengi zaidi” alisema Mmuya.
Kwa upande wake Afisa Utumishi Mkuu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Lucy J. Timba, wakati akikabidhi zawadi ya kikombe na cheti kwa Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, alisema kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na halmashauri zake mbili wamefanya vizuri katika tuzo za umahili wa vitengo vya mawasiliano serikalini kwa utoaji wa habari kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Alisema kuwa katika tuzo hizo Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kilishika nafasi ya nne na kupewa zawadi ya kombe na cheti cha utambuzi. “Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmasahuri ya Jiji la Dodoma kilishika nafasi ya 13 na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Mji Kondoa kilishika nafasi ya 15 na wote kupewa zawadi ya cheti cha utambuzi” alisema Timba.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Hellen Minja alisema kuwa kitengo chake kimejipanga kupiga hatua zaidi. “Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma tunampango wa kufanya vizuri zaidi na kuwa washindi namba moja katika kuhabarisha umma nchini. Tutafanya kazi zaidi ya mwanzo ili tuwe bora” alisema Minja.
Tuzo ya umahili wa vitengo vya mawasiliano serikalini vilivyofanya vizuri kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ilitangazwa na Mkurgenzi wa idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 18 June, 2024 katika Kongamano la pili la maendeleo ya sekta ya Habari nchini lililohudhuriwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na zawadi kukabidhiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 21 June, 2024 katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.